Karata za David Cameron
5 Novemba 2015Kashfa ya kampuni ya Volks Wagen na madhara yake kwa makampuni mengine ya magari nchini Ujerumani,tishio la Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya na wakimbizi na jinsi watakavyoweza kusaidia katika huduma za jamii ni miongoni mwa mada magazetini.
Tunaanza na kashfa inayozidi kuikaba kampuni mashuhuri ya magari nchini Ujerumani-Volks Wagen.Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika:"Makampuni ya General Motors,Ford na mengine kadhaa yanayotengeneza magari ya mizigo yameshawahi katika miaka ya 90 kukabiliana na kishindo cha taasisi ya usafi wa mazingira ya Marekani EPA kwasababu ya kutumia chombo cha kughushi vipimo vya moshi wa sumu.Viongozi mjini Wolfsburg kwa hivyo walikuwa wakijua fika,kwa jinsi gani mchezo walioukusudia kuucheza ni wa hatari.Viongozi hao hawakutilia maanani walipokuwa wakipiga hesabu zao kwamba mazingira ya kisiasa yamebadilika nchini Marekani:kinyume na hali namna ilivyokuwa zamani,visa vya kuchafuliwa hali ya hewa haviangaliwi tena kama makosa madogo madogo.Volks Wagen wanaonekana wanazidi kuikuza kashfa hiyo.Taasisi ya Marekani ya usafi wa mazingira-EPA inalalamika dhidi ya ukosefu wa ushirikiano kutoka Ujerumani.Viongozi wa mjini Wolfsburg hawaonyeshi hamu ya kujibu masuala kadhaa kutoka Washington.Hilo linatisha.Wakati umewadia wa kuanzishwa mbinu za aina mpya na VW nchini Marekani-sio tu kwa kubuni vifaa vya aina mpya bali pia kwa kuwa na kundi jipya linalolijua vyema soko la Marekani.
Vitisho vya Uengereza kwa Umoja wa ulaya
Kitisho cha Uingereza kutaka kujitoa katika Umoja wa Ulaya kimechambuliwa na mhariri wa gazeti la mjini Koblenz la "Rhein Zeitung"anaeandika:"Cameron anaupekecha mhimili wa Umoja wa Ulaya-kufika hadi ya kutaka kuushawishi Umoja wa sarafu ambao nchi yake hata si mwanachama.Haya ni maajabu makubwa ya kuyaelewa mamlaka ambayo yeye binafsi anayapigania kwaaliji ya nchi yake lakini wengine anawakatalia.Waziri mkuu bora aache mchezo huo hatari.Kwasababu hata kama utayarifu wa nchi hiyo ya kifalme kusalia katika Umoja wa ulaya ni mkubwa,lakini sauti za wale wanaodai waingereza waachiwe wende,zinazidi pia kuhanikiza."
Sura halisi ya wajerumani na utu wao yajulikana
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mzozo wa wakimbizi na jinsi ya kuwahudumia ipasavyo.Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika:"Anaehitaji msaada,anabidi apewe-huo ni muongozo wa kidini na ambao hapa unaweza kutekelezeka kwa namna mbili.Kwasababu msaada unatolewa na jeshi la shirikisho Bundeswehr na sio tu kwa wakimbizi bali pia kwa wale wasaidizi ambao ni wengi na ambao wanawajibika kupindukia uwezo wao kimwili na kisaikolojia.Na hiyo ndio picha halisi ya Ujerumani ya mwaka 2015-na sio ile ya wenye dhana mbovu dhidi ya wale wanaohitaji kuhifadhiwa.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu