Kansela Merkel ziarani Uturuki
30 Machi 2010Uanachama wa Uturuki katika Umoja wa Ulaya ni mada iliyo muhimu kabisa kwa nchi hiyo na pia hilo ni suala tete. Uturuki imevunjika moyo kwa kuzorota utaratibu wa kujiunga katika Umoja wa Ulaya. Pendekezo la Kansela Merkel kuwa Uturuki badala yake iwe na ushirikiano wa aina pekee pamoja na nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya umepuuzwa na Uturuki ikishikilia kuwa majadiliano yaliyoanzishwa yanahusika na uanachama kamili na sio kingine cho chote. Kuhusu suala hilo Kansela Merkel amesema:
CLIP: MERKEL
Merkel akaongezea kuwa mazungumzo ya uanachama lakini yameleta mageuzi ya kuvutia nchini Uturuki. Hata hivyo, masuala yanayohusika na Cyprus ni lazima kupatiwa ufumbuzi.
Tofauti za maoni ziliibuka pia katika suala linalohusika na mradi wa nyuklia wa Iran.Erdogan amesema kuwa Uturuki haiungi mkono kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi kama njia ya kuishinikiza kuhusu mpango wake wa nyuklia. Kwa maoni ya Uturuki, vikwazo sio njia ya maana kuutenzua mgogoro huo, bora zaidi ni kutumia njia za kidiplomasia.
Uturuki ni mwanachama wa muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Erdogan amesema nchi yake bado haijaamua vipi itapiga kura juu ya azimio la kuiwekea Iran vikwazo. Azimio hilo linahimizwa na Marekani na nchi za Magharibi zikiwa na wasiwasi kuwa Iran ina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia kwa siri.
Merkel ameishinikiza Uturuki kuwa tayari kuunga mkono azimio hilo ikiwa Iran haitoihakikishia jumuiya ya kimataifa kuwa haina njama ya kutengeneza silaha za nyuklia. Uturuki lakini haina hakika iwapo vikwazo vitakuwa na maana.
Hii leo Kansela Merkel anamaliza ziara yake mjini Istanbul ambako atakutana na wafanyabiashara wa Uturuki na Ujerumani.
Mwandishi: Martin,Prema/RTRE/DPA
Mhariri:Hamidou,Oummilkheir