1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel wa Ujerumani ahitimisha ziara yake nchini India.

1 Novemba 2007

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amehitimisha leo ziara yake ya kwanza nchini India.

https://p.dw.com/p/C77K
Waziri mkuu was India, Manmohan Singh (kulia), akimkaribisha Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel
Waziri mkuu was India, Manmohan Singh (kulia), akimkaribisha Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela MerkelPicha: AP

Wacha huko Berlin matatizo makubwa ya kisiasa yamgojee Kansela Angela Merkel kuyashughulikia, lakini katika siasa za kigeni bibi huyo anaweza kutamba kwamba anapata mafanikio. Lazima mtu ampe haki kwamba ameivunja ile siasa ya muda mrefu ya Ujerumani kuelekea Asia ambayo ilijishughulisha sana na China, na sasa anaielekeza zaidi kuelekea India. Hatua hiyo ingefaa ingechukuliwa muda mrefu uliopita. Lakini ilikuwa yule aliyekuwa waziri wa uchumi, Manmohan Singh ambaye mwanzoni mwa miaka ya tisini aliyejichagulia njia ya kuyafungua masoko ya India kwa nchi za nje na kuongoza mbio za India za kuukimbilia wakati ilioupoteza hapo kabla. Mbio hizo sasa zinawashangaza Wajerumani, licha ya kwamba nao pia wamechelewa kuzingudua. Akiwa sasa waziri mkuu, Manmohan Singh ameipandisha hadhi ya ziara hii ya kansela Angela Merkel kutoka kuwa, kama ilivopangwa mwanzo, ziara ya kikazi na kuwa ziara ya kiserekali. Hivyo kuweka msingi wa ziara hiyo kufaulu.

Kama nchi ilio maskini, tena yenye makabila mbali mbali, India kwa zaidi ya nusu karne imejitolea kufuata mfumo wa demokrasia. Hilo peke yake linafaa tangu zamani kupongezwa. Huko New Delhi na Bombay, Angela Merkel kila wakati alisisitiza kwamba India na Ujerumani zimefungamana katika kutetea thamani za pamoja, kama vile kuheshimu haki za binadamu, dola kufuata utawala wa seria na kuwa na demokrasia, kinyume na nchi nyingine kubwa katika Asia. Uchina inaweza sasa ikahisi na kufahamu kwamba kuegemea huku kwa Ujerumani upande wa India ni kuitenga Uchina, jambo ambalo Angela Merkel kabisa halitaki, lakini ni lazima alikubali. Kupanda kwa haraka uchumi wa India kunasababisha kupanuka pengo la neema baina ya tabaka mpya ya katikati na watu wengi sana walio bado maskini hohe hahe, ambao ni thuluthi moja ya wananchi. Hali hiyo pia mtu anaijuwa huko Uchina, lakini kwa kukosekana demokrasia nchini humo, mivutano inaweza kuwa ya hatari zaidi. Jambo hilo aliliweka wazi Angela Merkel. Hajafanya hiyvo hadharani, lakini aliweka wazi faraghani kwa wenyeji wake, pale milango ya vyumba ilipokuwa imefungwa.

Bila ya shaka, Angela Merkel hajaweza kuyapata yote aliyoyaendea huko India. Juu ya mazungumzo ya Doha kuhusu kupatikana muwafaka wa mfumo wa bishara duniani, bado ziko tafauti baina ya India na Ujerumani. Pia katika suala la ulinzi wa hali ya hewa bado kuna pengo la kutofahamiana baina ya India na Ujerumani. Lakini katika masuala haya mawili ya kimataifa, mazungumzo baina ya waziri mkuu Manmohan Singh na Kansela Angela Merkel yamesukuma mbele ile nia halisi ya pande hizo mbili kutaka kuchangia kupatikana suluhisho. Ikiwa mwishowe jambo hilo litawezekana basi mtu itamlazimu aitathmini ziara ya Kansela Angela Merkel huko India, licha ya kwamba imechelewa kufanyika, kuwa ya mafanikio.