1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa la Coptic laadhimisha Krismas chini ya ulinzi mkali

Admin.WagnerD7 Januari 2011

Magari ya jeshi yenye silaha yamewekwa karibu na makanisa nchini Misri leo (7 Januari 2011) wakati madhehebu ya Coptic wakisherehekea sikukuu ya Krismas, siku chache baada ya shambulio la bomu lilioua watu 21.

https://p.dw.com/p/zufs
Mtoto wa Rais Hosni Mubaraka, Gamal Mubarak (katikati), akishiriki misa ya Mkesha wa Krismas katika kanisa Coptic mjini Cairo, Misri, Alhamis Jan. 6, 2011.
Mtoto wa Rais Hosni Mubaraka, Gamal Mubarak (katikati), akishiriki misa ya Mkesha wa Krismas katika kanisa Coptic mjini Cairo, Misri, Alhamis Jan. 6, 2011.Picha: AP

Watu wenye magari wamepigwa marufuku kuegesha magari yao mbele ya makanisa, ambayo usalama wao unaangaliwa kwa kina na vikosi vya wataalamu wa kugundua mabomu pamoja na polisi. Kwa kalenda ya waumini wa madhehebu ya Coptic, sikukuu ya Krismas inaangukia tarehe 7 Januari.

Baadhi ya Waislamu wamejitokeza katika makanisa kuweka uzio wa binadamu kuzuwia chochote kinachoweza kutokea, ikiwa ni kuonyesha mshikamano na jamii ya waumini wa madhehebu ya Coptic nchini Misri, ambao hushambuliwa mara kwa mara, na ambao ni asilimia 10 ya wakaazi wapatao milioni 80 nchini humo.

Hatua hizo zimechukiwa wakati Wakristo wa madhehebu ya Coptic nchini Misri wakihudhuria misa ya mkesha wa Krismas jana Alhamis, makanisa yao yakiwa yamezingirwa na uzio wa chuma uliowekwa na majeshi ya usalama. Maafisa wa usalama wamesema kuwa kiasi cha polisi 70,000 wamewekwa nchi nzima kuhakikisha usalama katika makanisa wakati waumini hao wa madhehebu ya Coptic wakihudhuria misa ya mkesha wa Chrismas.

Papa Shenouda III wa Kanisa la Coptic akiongoza misa ya mkesha wa Krismas katika kanisa la madhehebu hayo mjini Cairo, Misri, Alhamis Jan. 6, 2011.
Papa Shenouda III wa Kanisa la Coptic akiongoza misa ya mkesha wa Krismas katika kanisa la madhehebu hayo mjini Cairo, Misri, Alhamis Jan. 6, 2011.Picha: AP

Polisi wamesema kuwa bomu dogo lililotengenezwa kienyeji, kwa kutumia kopo lililowekwa misumari na vipande vya chuma, lakini bila ya chombo cha kukiripua, limegunduliwa katika kanisa katika mji wa kusini wa Minya.

Gazeti rasmi la serikali Al-Ahram limeripoti kuwa ulinzi pia umeongezwa katika maeneo ya kitalii.

Wakati huo huo, makanisa manne ya Coptic mjini Sydney, nchini Australia, yamepokea vitisho vya kushambuliwa katika wakati waumini wa kanisa hilo wakijitayarisha kwa misa ya mkesha wa Krismas, wameeleza polisi wa nchi hiyo. Wale waliohudhuria misa ya mkesha wa Krismas jana Alhamis mjini Sydney wamesema kuwa polisi wamekuwa wakifanya upekuzi kutafuta mabomu , na helikopta za polisi zilikuwa zikiruka juu angani.

Kiongozi wa muungano wa Waislamu nchini Ujerumani amehudhuria misa ya mkesha wa Krismas jana katika kanisa la Coptic , katika ishara ya mshikamano na karibu Wakristo 23 waliouwawa katika shambulio la bomu nchini Misri. Kiongozi wa kanisa la Coptic mjini Frankfurt, Michele Riad, amesema kuwa polisi wamehakikisha kuna usalama wa hali ya juu wakati misa ya mkesha wa Krismas inafanyika.

O-Ton Michele Riad

Kwa upande mmoja, tunamuamini Mwenyezi Mungu. Na kwa upande mwingine tuko pamoja na jamii ya Wajerumani ambao tunawaamini. Polisi wapo na wanatulinda, kwa hiyo tumo katika usalama wa hali ya juu.

Viongozi wa kanisa Katoliki na la Kiluteri nchini Ujerumani pia wamesema hapo kabla kuwa watahudhuria misa hiyo. Makanisa mengi ya mataifa ya eneo la mashariki ya Ulaya yanayofuata madhehebu ya Kikristo ya Othordox, yanafuata kalenda tofauti na inayofuatwa na makanisa ya nchi za magharibi, ikiwa na maana kuwa kwa wao Krismas inaadhimishwa karibu wiki mbili baadaye.

Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE / DPAE

Mhariri : Miraji Othman