1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya Al Shabaab yashambuliwa Somalia

5 Oktoba 2013

Kundi la wanamgambo wa Al Shabaab limedai kuwa mpiganaji wao mmoja ameuwawa kusini mwa Somalia Jumamosi(05.10.2013) kufuatia shambulio la usiku kwenye mji wa Barawe linalodaiwa kufanywa na vikosi vya nchi za magharibi.

https://p.dw.com/p/19uDe
Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia.
Wapiganaji wa Al-Shabaab nchini Somalia.Picha: AP

Kwa mujibu wa vikosi vya usalama vya Somalia na wakaazi wa mji huo idadi isiojulikana ya wanamaji na wanajeshi wa anga walifanya shambulio hilo wakati wa usiku katika mji wa Barawe ulioko kilomita 180 kusini mwa mji mkuu wa Somalia Mogadishu.Msemaji wa Al-Shabaab Sheikh Abdi'asis Abu Muscab amekiambia kituo cha radio cha Andulus kwamba vikosi vya kigeni vikiwa na helikopta na boti za mwendo wa kasi vilivamia baadhi ya kambi zao katika mji wa Barawe asubuhi hii na kumuuwa mpiganaji wao mmoja shujaa na kujeruhi wengine kadhaa lakini wamewashinda wavamizi hao.

Wakaazi wa Barawe wamethibitisha kwamba helikopta kadhaa zilikuwa zikiruka juu ya mji huo usiku kucha.Mkaazi mmoja ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwa sharti ya kutotajwa jina lake kwamba kulikuwako na shambulio la anga lililoilenga nyumba ya Al Shabaab katika sehemu mojawapo ya mji huo na kwamba wamesikia sauti ya mapigano ya risasi yaliodumu kwa takriban saa nzima.

Ameongeza kusema kwamba hawana uhakika watu wangapi wameuwawa katika shambulio hilo lakini wameambiwa kwamba takriban wapiganaji watano wa Al Shabaab wameuwawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa.Wanamgambo wengine wawili imeripotiwa kuwa wamekufa baadae Jumamosi.

Habari zinatatanisha

Maafisa wa usalama wa Somalia wamekuwa wakitoa taarifa za kutatanisha kuhusu shambulio hilo.

Mji wa Barawe ulioko kusini mwa mji mkuu wa Mogadishu.
Mji wa Barawe ulioko kusini mwa mji mkuu wa Mogadishu.

Afisa wa ujasusi aliyeko Mogadishu aliyejitaja kwa jina la Mohamed ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba wanachofahamu ni kuwa vikosi vya Ufaransa vimemjeruhi Abu Diyad ambaye pia anajulikana kama Abu Ciyad kiongozi wa Al Shabaab kutoka Chechnya na kumuuwa mlinzi wake mkuu ambaye pia alikuwa ni raia wa kigeni.Amesema shambulio hilo lilikuwa hasa limemlenga kiongozi huyo wa Al Shabaab kutoka Chechnya.

Jeshi la Ufaransa hapo awali lilisema kwamba halikuhusika katika shambulio hilo.

Afisa mwengine wa ujasusi amesema shambulio hilo la Barawe limefanywa na vikosi vya Marekani na kuthibitisha kwamba lilikuwa limemlenga raia wa kigeni na pia raia mwengine wa kigeni alijeruhiwa katika shambulio hilo.

Hapo mwaka 2009 helikopta zilizokuwa na kikosi maalum cha Marekani walimuuwa mwanamgambo mwandamizi wa Al Qaeda Saleh Ali Saleh Nabhan katika shambulio kusini mwa Somalia.Nabhan alikuwa akituhumiwa kutengeneza bomu ambalo limeuwa watu 15 kwenye hoteli inayomilikiwa na Israel katika mwambao wa Kenya hapo mwaka 2002.

Saleh Ali Saleh Nabhan mwanamgambo wa Al Qaeda aliyeuwawa na kikosi cha Marekani.
Saleh Ali Saleh Nabhan mwanamgambo wa Al Qaeda aliyeuwawa na kikosi cha Marekani.Picha: AP

Jumuiya ya Kujihami ya NATO na kikosi cha Umoja wa Ulaya cha kupambana na uharamia Navfor nje ya mwambao wa Somalia zimekanusha kuhusika na shambulio hilo la Barawe.

Halikuwa shambulio la anga

Akielezea zaidi kuhusu shambulio hilo Musab msemaji wa Al Shabaab amesema helikopta wala ndege hazikushiriki katika shambulio hilo na kwamba walivamiwa na vikosi vya nchi za magharibi vikiwa kwenye maboti na waliweza kuvitimua na kuacha nyuma silaha, madawa na alama za damu.

Wapiganaji wa Al Shabaab wakiwa katika mafunzo Somalia.
Wapiganaji wa Al Shabaab wakiwa katika mafunzo Somalia.Picha: picture-alliance/AP

Amesema ingawa wote walitumia maguruneti kushambuliana, washambuliaji walikuwa na silaha zisizotowa sauti na kwamba milio ya silaha iliosikika ilikuwa ni yao.

Wakaazi wamesema mapigano hayo yalizuka saa tisa alfajiri.Sumira Nur mama wa watoto wanne ameliambia shirika la habari la Reuters hapo Jumamosi kutokea Barawe kwamba waliamshwa na milio mizito ya risasi wakati wa usiku na walidhani kambi ya Al Shabaab ilioko ufukweni imetekwa.

Marekani huko nyuma ilitumia ndege zisizokuwa na rubani kuuwa wapiganaji nchini Somalia.Hapo mwezi wa Januari mwaka 2012 kikosi maalum cha wanamaji wa Marekani cha SEAL kiliwaokowa wafanyakazi wawili wa shughuli za misaada baada ya kuwauwa watekaji wao tisa.

Hapo mwezi wa Januari mwaka huu jeshi la Ufaransa lilitumia helikopta kushambulia kambi ya Al Shabaab katika kijiji cha kusini kumuokowa mateka mmoja wa Ufaransa. Makomandoo wawili wa Ufaransa waliuwawa na waasi baadae walidai kuwa wamemuuwa mateka huyo waliokuwa wakimshikilia.

Ufaransa imesema haikushiriki katika shambulio hili jipya.

Haikuweza kufahamika iwapo shambulio hilo linahusiana na shambulio la jengo la kibiashara nchini Kenya wiki mbili zilizopita ambalo kundi hilo la Al Shabaab lenye mafungamano na kundi la Al Qaeda limedai imelitekeleza na kuuwa watu 67.

Jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi liliposhambuliwa na wanamgambo wa Al Shabaab.
Jengo la kibiashara la Westgate mjini Nairobi liliposhambuliwa na wanamgambo wa Al Shabaab.Picha: Reuters

Kiongozi wa Al Shabaab Ahmed Godane ambaye anajulikana kwa jina la Mukhtar Abu al-Zubayr amesema shambulio hilo lilikuwa ni kulipiza kisasi kwa hatua ya Kenya kupeleka vikosi vyake kusini mwa Somalia hapo mwezi wa Oktoba mwaka 2011 kuzima uasi wa kundi lao.

Barawe inadhibitiwa kikamilifu na wanamgambo wa kundi hilo la itikadi kali za Kiislamu.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa

Mhariri: Bruce Amani