Kagawa ataihama Dortmund au haondoki?
4 Mei 2012Kagawa ambaye ameshinda taji la Bundesliga mfululizo tangu alipojiunga na Dortmund kwa kima cha euro 350,000 pekee kutoka klabu ya daraja la pili huko Japan, ameridhisha vya kutosha na kumezewa mate na vilabu kadhaa vikuu yva Ulaya.
Mkataba wa Mchezaji huyo wa Japan unakamalikika mwaka wa 2013 na Kagawa tayari wakati mmoja amewahi kuelezea hamu yake ya kucheza soja yake Uingereza. Kagawa ambaye amefunga magoli 13 katika ligi ameliambia gazeti la Ujerumani Bild kuwa kuwa hajaamua cha kufanya.
Jupp na Robben kusalia Bayern
Jupp Heynckes amesema atasalia kama kocha wa Bayern Munich hata ikiwa timu yake itashinda kombe la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Chelsea katika fainali ya tarehe 19 Mei uwanjani Allianz Arena.
Heynckes mwenye umri wa miaka 66 na vyombo vya habari vya Ujerumani vimeeneza uvumi kuwa huenda akajiuzulu ikiwa Bayern itashinda. Kocha huyo ana mwaka mmoja zaidi katika mkataba wake wa sasa na amewaambia waandishi habari kuwa atasalia katika klabu hiyo. Bayern inamaliza katiia nafasi ya pili katika ligi ya Bundesliga na itacheza fainali ya kombe la Shirikishi dhidi ya mabingwa Dortmund.
Arjen Robben ameurefusha mkataba wake na klabu ya Bayern Munich hadi mwaka wa 2015 licha ya mzozo ulizuka baina yake na mwenzake Franck Ribery wakati wa mchuano wa Ligi ya Mabingwa.
Wachezaji hao wawili walizozana wakati wa kipindi cha mapumziko katika mchuano wa mkondo wa kwanza walioshinda magoli mawili kwa moja dhidi ya Real Madrid. Hali hiyo ilimchelewesha Robben kusaini mkataba huo. Lakini Bayern imesema Robben mwenye umri wa miaka 28 raia wa Uholanzi amesaini kuurefusha kwa miaka miwili zaidi na kuuondoa wasiwasi wowote kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Robben anasema anahisi vizuri kuwa katika klabu hiyo kwa sababu Bayern ni kama familia yake.
Capello ataka kurejea Uingereza
Kocha wa zamani wa Uingereza Fabio Capello anataka kurejea katika mambo ya soka kwa kujiunga na mojawapo ya vilabu vikuu katika ligi ya Uingereza. Capello ameliambia gazeti la The Times kuwa Uingereza itakuwa nzuri kwake kwa sababu nazifahamu timu na wachezaji vizuri. Capello mwenye umri wa miaka 65 anasema anataka kuifunza timu inayotaka kushinda mataji.
Muitaliano huyo ambaye alijiuzulu kama kocha wa Uingereza mwezi Februari aliongeza kuwa hafanyi kazi kwa sababu ya pesa. Ameshawahi kuzifunza timu za AS Roma, AC Milan, Juventus na Real Madrid.
Capello anaunga mkono hatua ya shirikisho la soka Uingereza FA kumchagua Roy Hodgson kama kocha mpya wa timu ya taufa ya The Three Lions, na amemtakia kila la kheri anapoanza kutekeleza majukumu yake.
Di Matteo anatosha
Nahodha wa Chelsea John Terry amempigia upatu meneja wake Roberto Di Matteo kupewa wadhifa huo kwa mkataba wa kudumu. Di Matteo amesajili matokeo ya kuridhisha tangu alipochukua usukani kutoka kwa meneja aliyepigwa kalamu Andre Villas-Boas mwezi Machi, na kuiongpza klabu hiyo hadi fainali ya kombe la FA na Ligi ya Mabingwa. Ijapokuwa matokeo ya Chelsea katika ligi ya nyumbani yanaonekana kuyumbayumba, huku klabu hiyo iking'ang'ana kumaliza katika nne bora, Terry amesifu hatua iliyopigwa na Di Matteo katika kipindi kifupi.
Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Othman Miraji