1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson alaani ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji

12 Julai 2021

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amelaani ubaguzi wa rangi uliojitokeza katika mitandao ya kijamii dhidi ya wachezaji wa England baada ya timu hiyo kushindwa na Italia katika fainali ya kuwania kombe la Euro 2020. 

https://p.dw.com/p/3wMHv
Großbritanniens Premierminister Boris Johnson über Lockerungen der Corona-Beschränkungen
Picha: DANIEL LEAL-OLIVAS/AFP

Polisi nchini Uingereza imesema itachunguza matusi na maneno ya ubaguzi wa rangi yaliyoandikwa katika mitandao ya kijamii dhidi ya wachezaji watatu wa England waliolengwa kwenye kadhia hiyo ambao wana asili ya Afrika Marcus Rashford, Jardon Sancho na Bukayo Saka.

Wachezaji hao walipoteza mikwaju ya penalti baada ya Italia na England kutoka sare bao 1-1 usiku wa kuamkia leo, mechi iliyochezwa katika uwanja wa Wembley mjini London mbele ya mashabiki 60,000 wengi wakiwa wanashabikia England. Kupitia mikwaju hiyo ya penalti Italia iliibuka na ushindi kwa mabao 3-2.

Soma pia Italia yauwa ndoto za England

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Boris Johnson amesema timu ya taifa England yapaswa kusifiwa kama mashujaa na si kutupiwa kauli za ubaguzi wa rangi. Johnson ameongeza kuwa waliohusika kwa ubaguzi huo wa kushangaza wanapswa kuona aibu wenyewe.

Mlinda lango wa Italia Gianluigi Donnarumma akizuia mkwaju wa penalti wa Bukayo Saka wa England.
Mlinda lango wa Italia Gianluigi Donnarumma akizuia mkwaju wa penalti wa Bukayo Saka wa England.Picha: Paul Ellis/Getty Images/AFP

Upigaji goti uwanjani kulaani ubaguzi wa rangi

Timu ya England imekuwa ikiangazia na kupinga suala la ubaguzi wa rangi tangu michuano ya kuwania kombe la mataifa ya bara Ulaya Euro 2020 ilipoanza kwa kupiga magoti uwanjani kila kabla ya mechi kuanza. Hata hivyo baadhi ya mashabiki waliwasuta kwa kitendo hicho, huku wakosoaji wakitizama kitendo hicho kama hatua ya kuingiza siasa kwenye michezo na vilevile ishara ya kuegemea siasa kali za mrengo wa shoto nchini humo.

Baadhi ya mawaziri wenyewe wameshutumiwa kuwa wanafik kwa kushindwa kuwakemea wale mashabiki walioikejeli  timu hiyo ilhali sasa wako mstari wa mbele kukemea visa vya ubaguzi wa rangi.

Waziri wa Mambo ya ndani nchini humo Priti Patel ambaye mwezi uliopita alisema haungi mkono hatua ya timu ya England kupiga goti uwanjani kwa sababu ni ishara  ya kisiasa, amesema amesikitishwa mno kwamba wachezaji wa England ambao walijitolea kwa njia zote kwa nchi yao katika mechi hizo, wamekabiliwa na ubaguzi wa rangi mitandaoni.

Southgate awatetea wachezaji wake

Kocha wa England Gareth Southgate akisalimiana na mchezaji wake Bukayo Saka Julai 7, 2021 wakati England ilipochuana na Denmark kwenye mechi ya nusu fainali Euro 2020.
Kocha wa England Gareth Southgate akisalimiana na mchezaji wake Bukayo Saka Julai 7, 2021 wakati England ilipochuana na Denmark kwenye mechi ya nusu fainali Euro 2020.Picha: Laurence Griffiths/REUTERS

Shirikisho la Kandanda la England (FA) nalo limetoa tarifa mapema leo likishutumu matukio hayo ya ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji Rashford, Sancho na Saka.

Kocha wa England Gareth Southgate, amewatetea wachezaji waliopoteza penalti akisema ndio walisalia nao wenye uweledi wa upigaji penalti. "Wanachopaswa kujua ni kwamba hawako peke yao. Tunashinda kama timu na kushindwa pia kama timu. Mimi ndio nilichagua wapigaji penalti. Tumewafanyia kazi mazoezini. Huo ni uamuzi wangu si wa wachezaji. Leo mambo hayakuwa upande wetu, lakini twajua ndio walikuwa bora tuliosalia nao uwanjani," amesema Southgate

Shirikisho hilo limesema limesikitishwa na kushangazwa na kitendo hicho cha kuaibisha na ambacho hakiruhusiwa dhidi ya timu. Limeongeza kuwa litafanya kila liwezalo kuwaunga mkono wachezaji walioathiriwa huku likihimiza adhabu kali itolewe kwa yeyote atakayepatikana na hatia.

Timu ya England pia ilitoa tarifa kulaani ubaguzi wa rangi ulioelekezwa dhidi ya wachezaji wao katika mitandao ya kijamii

Meya Sadiq Khan ataka kampuni za mitandaoni kukabili chuki

Meya wa mji wa London Sadiq Khan kupitia ukurasa wake wa Twitter, ametoa mwito kwa kampuni za mitandao ya kijamii kuondoa matusi na maudhui yote ya ubaguzi wa rangi kwenye mitandao yao haraka iwezekanavyo na kuzuia chuki kama hizo.

Suala hilo la ubaguzi wa rangi dhidi ya wachezaji, lilisababisha maafisa wa soka nchini Uingereza kusitisha na kususia kwa muda mitandao ya kijamii kama hatua ya kuangazia kadhia hiyo. Hatua iliyoungwa mkono na mashirika mengine ya michezo.

Mchezaji wa ENgland Marcus Rashford akionekana amevunjika moyo baada ya timu yao kushindwa na Italia katika fainali za Euro 2020 katika uwanja wa Wembley Julai 11, 2021.
Mchezaji wa ENgland Marcus Rashford akionekana amevunjika moyo baada ya timu yao kushindwa na Italia katika fainali za Euro 2020 katika uwanja wa Wembley Julai 11, 2021.Picha: John Sibley/REUTERS

Kampuni za mitandao ya kijami imelaumiwa mara kwa mara kushindwa kushughulikia kadhia hiyo ipasavyo.

Mnamo mwezi Mei, serikali ya Uingereza ilitangaza mipango ya sheria mpya ambayo huenda italazimisha kampouni za mitandao ya kijamii kupigwa faini ya hadi pauni milioni 18 ikiwa itashindwa kukabili uchochezi na ubaguzi wa rangi mitandaoni.

Ndoto ya England kutwaa ubingwa yazama

Vijana wa England walianza kwa kasi kupitia bao la dakika ya pili lake Luke Shaw lakini Italia ilidhihirisha umahiri wao waliposawazisha kupitia Leonardo Bonucci mnamo kipindi cha pili.

England ilitarajia kushinda mechi ya jana ili kumaliza ukame wao wa ushindi wa mataji makubwa tangu iliposhinda Kombe la Dunia mwala 1966.

Lakini hilo halikutimia. Kwa Italia huo ulikuwa ushindi mtamu baada ya kusubiri kwa muda mrefu kwani mara ya mwisho walilishinda kombe hilo ni mwaka 1968,

(RTRE, APE)