Jeshi la Ujerumani na wakimbizi Magazetini
29 Septemba 2014Tuanze lakini na hali katika jeshi la Ujerumani Bundeswehr ambalo linasemekana baadhi ya vifaa vyake haviambatani na wakati,likizuka suala kama linaweza kutekeleza majukumu yake katika daraja ya kimataifa.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:
"Bila ya Shaka Ursula von der Leyen sio peke yake anaebeba dhamana ya hali ya kusikitisha katika jeshi la shirikisho-Bundeswehr.Miaka nenda miaka rudi waliomtangulia walikuwa wakifuata ule usemi "funika kombe mwanaharamu apite".Hata hivyo von der Leyen anaweza kulaumiwa kwamba hakutekeleza wajibu wake. Kwa sababu jukumu kubwa mtu anapokabidhiwa wadhifa wa waziri ni kujua kwanza kilichoko.Badala ya kuonya aliahidi kwa pupa ataligeuza jeshi la Ujerumani kuwa tasisi ya kimambo leo ya kuwaajiri watu.Msimu wa kiangazi yakafuata madai ya kuwajibika zaidi kijeshi Ujerumani ulimwenguni.Hivi sasa inabainika bila ya msaada kutoka kwa washirika wake,jeshi la Ujerumani haliwezi hata kufika mahala linakobidi kutekeleza majukumu yake.Hali hii lazima isawazishwe haraka ili kujiepusha na aibu."
Gazeti la "Freie Presse lina maoni mengine kabisa.Gazeti linaandika:"Sio kila nchi mwanachama wa Umoja wa ulaya ingelazimika kuwa na uwezo mkubwa wa kukidhi mahitaji ya kijeshi kama Umoja wa Ulaya wenyewe ungekuwa na sera ya pamoja ya ulinzi na usalama.Mizozo nchini Ukraine na pia kitisho kinachotokana na wafuasi wa itikadi kali wa dola la kiislam-IS inabainisha umuhimu kwa Umoja wa Ulaya kuwa na sauti moja pia katika sekta ya kijeshi ili kutetea ipasavyo fikra ya umoja huo linapohusika suala la uhuru na demokrasia."
Sera za Mazingira za Ujerumani zimepungua makali
Sera za mazingira za Ujerumani zilizokuwa zikisifiwa ulimwenguni, zimepwaya-linaandika gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" na kuendelea:"Enzi ambapo mapambano dhidi ya kuzidi hali ya ujoto duniani na kupunguza moshi wa sumu unaotoka viwandani na kuchafua mazingira yalikuwa yakipewa umuhimu mkubwa-zimepita."Kansela mpigania hifadhi ya mazingira",Angela Merkel ambae mwaka 2007,alipokuwa mwenyekiti wa kundi la mataifa manane tajiri kiviwanda G-8 aliiorodhesha mada hiyo katika ajenda ya mkutano,anaonyesha kutoshughulishwa tena na masuala hayo.Masuala ya tabia nchi yanashughulikiwa na wizara maalum-lakini si miongoni mwa vigogo serikalini."
Laana baada ya wakimbizi kunyanyaswa
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu laana zilizotolewa kufuatia picha zilizochapishwa na kuonyesha jinsi wakimbizi wanavyotendewa maovu.Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:
"Kinachoudhi zaidi katika picha hizo zinazoonyesha jinsi mtumishi wa shirika la kibinafsi la usalama,alivyokuwa akiwanyanyasa wakimbizi katika kituo cha kuwapokea wakimbizi,sio pekee maovu yenyewe yasiyokuwa na mfano,bali zaidi ile hali kwamba hakuna anaeshuku kama picha zile si za kweli na kwamba binaadamu wanaweza kufanya visa vya kinyama kama vile.Wakati umewadia wa kuwafumbua waatu macho:matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya wanaoomba kinga ya ukimbizi,kuvurumisha mawe dhidi ya vituo wanakoishi wakimbizi,matamshi ya chuki yote hayo yanawapa nguvu wafuasi wa itikadi kali waliojaa chuki na ambao ndio sababu ya watu kuyapa kisogo maskani yao.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga