1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji huo umekuwa ngome ya majeshi ya Mashariki ya LNA

Faiz Musa27 Juni 2019

Jeshi tiifu kwa serikali ya Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Libya limechukua uthibiti wa mji wa Gharyan - kusini mwa Tripoli, mji ambao umekuwa ngome ya majeshi ya Mashariki yanayoishambulia Tripoli.

https://p.dw.com/p/3LAXh
Libyen 2017 | Khalifa Hifter, General
Picha: picture-alliance/AP Photo/I. Sekretarev

Msemaji wa jeshi hilo la serikali ya makubaliano ya kitaifa, GNA, Mahammed Gannouno alisema wamevamia eneo la kati la mji wa Gharyan na kuchukua uthibiti wa taasisi zake na kuwashinda wanajeshi wa mbabe wa kivita Khalifa Haftar. Nalo baraza la raisi lililo na mamlaka na serikali ya Tripoli limetoa taarifa likieleza kwamba mji huo ulikombolewa kabisa kutoka kwa jeshi tiifu kwa Haftar, LNA, na mjumbe mmoja wa baraza hilo Mohammed Al-Ammari katika taarifa tofauti amewaonya LNA dhidi ya kulipiza kisasi.

darzeni kadhaa za wanajeshi wa Haftar waliuliwa na wengine 18 walikamatwa kama wafungwa. Picha zilienezwa katika mitandao ya kijamii ya jeshi la GNA wakishika doria katika mji huo na vile vile wakionekana kuwakamata wafungwa hao.

Duru za kijeshi kutoka kwa upande wa Haftar zilieleza kwamba kumekuwa na usaliti kutoka kwa vikosi vya siri vilivyowaruhusu wanajeshi wa Tripoli kuingia katika mji wa Gharyan kilomita mia moja upande wa kusini mwa Tripoli. Mbabe wa kivita aliyejitangGannounoazia serikali yake ya LNA, Khalifa Haftar alikuwa akiudhibiti mji huo tangu April baada ya kuanzisha mashambulizi ya kuunyakua mji mkuu wa Tripoli kutoka kwa serikali ya makubaliano ya kitaifa, GNA.

Infografik Karte Libyen Gharyan DE
Ramani inayoonyesha mji wa Gharyan

Pigo kwa Khalifa Haftar 

Kuchukuliwa kwa mji huo ni pigo kubwa kwa Haftar japo bado ana uthibiti wa mji wa Tarhouna ulioko kusini mwa Tripoli ambapo ni sehemu yake muhimu ya pili katika kampeni yake hiyo. 

Mtaalamu wa maswala ya sera katika shirika la Kazkazini Afrika na Mashariki ya Kati katika baraza la Ulaya juu ya mahusiano ya kigeni, Tarek Megerisi, alisema mji wa Gharyan kurudi chini ya mamlaka ya serikali ya GNA ni mabadiliko muhimu sana na iwapo Haftar atafanikiwa kuuchukua tena - japo kuna mashaka ya kufanya hivyo - basi mji wa Tarhouna na sehemu nyengine zilizosalia katika jeshi lake la LNA vitapoteza uwezo na pia hawatakuwa na ari kubwa ya kufanya mashambulizi.

Haftar na wanaomuunga mkono wanadai wanajaribu kuwaondoa waasi kutoka mji mkuu wa Tripoli wanaowalaumu kwa kuyumbisha nchi ya Libya tangu kuangushwa kwa utawala wa marehemu Muammar Gaddafi na vuguvugu la mabadiliko lililoungwa mkono na vikosi vya NATO mwaka 2011. Wakosoaji wa Haftar wanamshutumu kwa kutaka kuchukua mamlaka ya Libya kwa kutumia nguvu hivyo kuzidisha mgogoro baina ya vikosi vya jeshi vilivyoko Mashariki na Magharibi mwa Libya.

(DPA/RTRE/AFPE)