1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yazuia kombora la masafa marefu kutoka Yemen

Angela Mdungu
15 Septemba 2024

Jeshi la Israel limesema kwamba limefanikiwa kulizuia kombora la masafa marefu lililorushwa kuelekea Tel Aviv likitokea Yemen Jumapili asubuhi. Kundi la Wahouthi la Yemen limekiri kuhusika na shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/4kdgj
Mzozo wa Mashariki ya Kati
Mtaalamu wa Israel akikifanyia uchunguzi kipande cha kombora lililorushwa ndani ya Israel kutoka Yemen Septemba 15.09.2024Picha: Ilia Yefimovich/dpa/picture alliance

Kulingana na jeshi la Israel, kombora lililorushwa lilitua katika eneo la wazi na hakuna taarifa zozote za uwepo wa majeruhi waliotokana na shambulio hilo.

Tukio hilo lilisababisha kulia kwa ving'ora ikiwemo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Israel na katikati mwa Tel Aviv. Jeshi limeeleza kuwa, milio ya milipuko iliyosikika ilitokana na kuzuiwa na mfumo wa kujilinda dhidi ya makombora.

Itakumbukwa kuwa, jeshi la anga la Israel liliushambulia mji wa bandari wa Hodeidah nchini Yemen mnamo mwezi Julai na kusababisha vifo vya watu sita.

Soma zaidi: Wahouthi wa Yemen waapa kulipiza kisasi shambulizi la Israel Hodeida

Lilifanya shambulio hilo baada ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kuushambulia kwa droni mji wa Tel Aviv mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa upande wake afisa habari wa waasi hao kupitia ukurasa wake wa X amesema kombora la Yemen lilifika Israel baada ya majaribio 20 ya nchi hiyo kushindwa kulizuia.