1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi la Israel lawataka wakaazi kuondoka Gaza

Angela Mdungu
13 Oktoba 2023

Jeshi la Israel limewaamuru Wapalestina wapatao milioni moja wanaoishi katika ukanda wa Gaza kuondoka kaskazini mwa mji huo. Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa amri hiyoinaweza kusababisha balaa kubwa.

https://p.dw.com/p/4XUjK
Mashambulizi ya Israel mjini Gaza
Mashambulizi ya Israel mjini GazaPicha: EYAD BABA/AFP

Agizo hilo la Israel limetolewa ikiwa ni siku saba tangu yalipoanza mapambano kati ya Israel na kundi la Hamas.

Kundi la Hamas lililofanya shambulio la kushtusha na la kikatili takribani wiki moja iliyopita, limewataka wakaazi wa Gaza kupuuza amri hiyo ya kuondoka kuelekea kusini mwa ukanda huo na kuitaja kuwa vita vya kisaikolojia.

Amri ya jeshi la Israel inayoulenga mji wa Gaza ambao ni makaazi ya maelfu ya raia na wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada imesababisha mkanganyiko kwa watu hao ambao tayari wanaukimbia mji huo kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel. Hadi sasa Ukanda huo uliozingirwa hauna huduma muhimu za kijamii ikiwemo umeme.

Soma zaidi: Vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza vyaingia siku ya saba

Agizo hilo linachukuliwa kama ishara nyingine ya mashambulizi ya ardhini yanayotarajiwa ingawa Israeli bado haijatangaza uamuzi huo. Jeshi la Israel hata hivyo limekiri mapema leo kuwa, itachukua muda kwa raia wa Palestina kuondoka,  na halikuthibitisha ripoti ya awali ya Umoja wa Mataifa kuwa imetoa saa 24 kwa wakaazi hao kuondoka Gaza.

Jana Alhamisi, jeshi hilo lilisema kuwa limejiandaa na liko tayari kwa operesheni ya ardhini kama litaamriwa kufanya hivyo.

Mashambulizi ya  aina hiyo kwenye eneo lenye msongamano la Gaza huenda yakasababisha kuongezeka kwa idadi kubwa ya majeruhi kutoka pande zote mbili za mzozo huo lakini serikali ya Israeli iko kwenye shinikizo kuhakikisha inalisambaratisha kundi la Hamas ambalo limeitawala Gaza tangu mwaka 2007.

Hamas: Mashambulizi ya Israel yamewaua mateka 13

Wakati agizo hilo likiendelea kuzua taharuki, Hamas imetangaza kuwa Waisrael 13 na mateka ambao ni raia wa mataifa mengine wameuwawa baada ya mashambulizi ya Israel katika mji wa Gaza. Licha ya kutoa taarifa hiyo wanamgambo hao wa Hamas hawakutaja uraia wa  watu hao wa mataifa mengine inayodai waliuwawa katika kipindi cha saa 24 zilizopita. 

Soma zaidi: Vita vya Gaza: Blinken afanya mazungumzo na Netanyahu

Awali, vikosi vya Ezzedine al-Qassam vilitahadharisha wiki hii kuwa, kila mashambulizi yatakayofanywa bila tahadhari na kuwauwa raia wa Gaza yatasababisha kuuwawa kwa mmoja wa raia waliochukuliwa mateka. Wanamgambo wa kundi la Hamas wamekuwa wakifanya shughuli zao katika makazi ya raia ambapo kwa muda mrefu Israel imewatuhumu kwa kuwatumia raia wa Palestina kama ngao.

Gaza baada ya mashambulizi ya Israel
Gaza baada ya mashambulizi ya IsraelPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi  bila kikomo Gaza yenye jumla ya wakaazi milioni 2.4 tangu shambulio la Jumamosi. Kwa mujibu wa ofisi ya habari ya Hamas mjini Gaza, kati ya waliouwawa kutokana na mashambulizi ya Israel yaliyosambaratisha majengo kwenye mji huo ni takriban watoto 500.

Vita kati ya Israel na Hamas viliibuka baada ya wapiganaji wa Hamas kuvamia kusini mwa Israel na kuwauwa mamia ya watu wakiwemo watoto na vijana waliokuwa katika tamasha la muziki Jumamosi iliyopita. Wanamgambo hao, pia wanawashikilia mateka watu wasiopungua 150 kutoka Israeli.

Hamas inazingatiwa na Marekani, Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani na baadhi ya mataifa mengine kuwa kundi la kigaidi.

Vyanzo: AP/AFP/REUTERS