Jeshi la Israel laondoka katika vijiji vya kusini, Lebanon
18 Februari 2025Waziri wa ulinzi wa Israel Israel Katz, amethibitisha leo kuwa wanajeshi wake wamesalia katika maeneo matano kusini mwa Lebanon baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho wa kuondoka nchini humo, huku akiahidi kuchukua hatua dhidi ya ukiukaji wowote wa makubaliano ya amani na kundi hilo la wanamgambo la Hezbollah.
Israel kuchukuwa hatua dhidi ya ukiukaji wowote wa Hezbollah
Katika taarifa, Katz amesema kuwa jeshi hilo la Israel litasalia katika eneo salama na kuwa na udhibiti wa maeneo matano ya kimkakati huku akiongeza kuwa litaendelea kuchukua hatua za nguvu dhidi ya ukiukaji wowote utakaofanywa na Hezbollah.
Lebanon yasema Israel lazima iondoke nchini mwake
Awali, chanzo kimoja cha usalama cha Lebanon, kililiambia shirika la habari la AFP kwamba jeshi la Israel limejiondoa katika vijiji vyote vya mpakani isipokuwa katika maeneo matano.
Wakati huo huo, jeshi la Lebanonlimetangaza kupeleka wanajeshi wake katika vijiji vya mpakani vilipoondoka vikosi vya Israel.
Miji na vijiji kadhaa vya mpakani, ikiwa ni pamoja na manispaa ya Mais al-Jabal, zilikuwa zimetoa wito kwa wakaazi waliokimbia makazi yao kusubiri hadi jeshi la Lebanon litakapochukuwa udhibiti wa maeneo hayo kabla ya kurejea, ili kuhakikisha usalama wao.
Lebanon: Rais mpya aibua matumaini ya utulivu Mashariki ya Kati
Mamlaka ya Lebanon imekataa kuongezwa tena kwa muda wa kujiondoa kwa vikosi vya Israel na kuwataka wafadhili wa makubaliano hayo kuishinikiza Israel kujiondoa.
Maandamano yafanyika Tel Aviv na Jerusalem
Watu jana walifanya maandamano mjini Tel Aviv na Jerusalem ikiwa imesalia muda wa chini ya wiki mbili kabla ya kukamilika kwa awamu ya sasa ya makubaliano ya amani kwaGaza.Mazungumzo kuhusu awamu ya pili ya mazungumzo hayo ya amani bado haijaanza.
Zaidi ya mateka 70 bado wanashikiliwa Gaza, huku karibu nusu wakihofiwa kuwa wamekufa.