1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Jeshi kuunda serikali ya mpito Bangladesh

5 Agosti 2024

Mkuu wa majeshi nchini Bangladesh Waker-Uz-Zaman amesema jeshi litaunda serikali ya mpito baada ya Waziri Mkuu Sheikh Hasina kujiuzulu na kuikimbia nchi.

https://p.dw.com/p/4j8Fd
Bangladesh | Jenerali Waker-Uz-Zaman
Mkuu wa majeshi wa Bangladesh, Jenerali Waker-Uz-Zaman.Picha: DW

Mkuu huyo wa majeshi ameongeza kuwa atatafuta mwongozo kutoka kwa rais wa nchi hiyo juu ya kuunda serikali mpya.

Akihutubia taifa baada ya kuondoka kwa Hasina, Jenerali Zaman alisema kuwa anachukua jukumu kamili, japo haijabainika wazi iwapo ataongoza serikali ya muda. 

Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Bangladesh akimbia nchi

"Waziri Mkuu amejiuzulu kutoka wadhifa wake na tutaunda serikali ya mpito kwa sasa kuiendesha nchi."

Zaman aliahidi kuwa watu wote waliouawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali watapata haki.

Zaman, aliyehitimu kutoka Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Bangladesh na ambaye aliwahi kuhudumu pia katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Angola na Liberia, ametoa mwito kwa maandamano kusitishwa.