1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yalenga kudhibiti maeneo yote ya kusini mwa Ukraine

23 Aprili 2022

Moscow inataka kuyadhibiti kikamilifu maeneo yote ya kusini mwa Ukraine, Jenerali wa Urusi amesema Ijumaa, tamko ambalo Ukraine imesema linakinzana na madai ya awali ya Urusi.

https://p.dw.com/p/4AKAJ
Ukraine-Krieg | Lage in Mariupol
Picha: Chingis Kondarov/REUTERS

Rustam Minnekayev, naibu kamanda wa wilaya kuu ya kijeshi ya Urusi, amanukuliwa na mashirika ya habari ya serikali ya Urusi akisema udhibiti kamili wa maeneo ya kusini mwa Ukraine ungeipatia njia ya kulifikia eneo lililojitemga na Moldova na linalokaliwa na Urusi katika upande wa magharibi.

Soma pia: Urusi yaonyesha utayari wa mazungumzo

Hiyo ingemaanisha kuikata pwani yote ya Ukraine na kusogea mamia ya maili upande wa magharibi mbali na misitari ya sasa, kupita miji mikubwa ya Ukraine ya Mykolaiv na Odesa.

Moscow inasema inaendesha "operesheni maalum ya kijeshi" kuivunja nguvu Ukraine kijeshi na kuwakomboa watu wake kutoka kile inachokiita wazalendo hatari. Ukraine na washirika wake wa Magharibi wanauita uvamizi wa Urusi kuwa ni vita vya uchokozi visivyo na msingi.

Ukraine | Kämpfer der tschetschenischen Spezialeinheit in Mariupol
Wapiganaji wa kikosi maalumu cha Wachechnya, wakiongozwa na mbunge wa bunge la Duma Adam Delimkhanov, wakitembea karibu na jengo la utawala la kiwanda cha Azovstal mjini Mariupol, Aprili 21, 2022.Picha: Chingis Kondarov/REUTERS

"Waliacha kukificha," wizara ya ulinzi ya Ukraine ilisema kwenye Twitter. Urusi ilikuwa "imekiri kwamba lengo la 'awamu ya pili' ya vita vyake siyo ushindi dhidi ya wanazi wa kufikirika, lakini ukaliaji wa mashariki na kusini mwa Ukraine. Ubeberu kama ulivyo."

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alikataa kuzungumza alipoulizwa iwapo Urusi imepanua malengo yake ya operesheni na namna Moscow inavyouona mustakabali wa kisiasa wa kusini mwa Ukraine. Afisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya alisema wiki mbili zijazo zinaonekana kuwa muhimu.

Soma pia: Marekani yaongeza msaada Ukraine, Urusi ikidai ushindi Mariupol

"Hii sio hadithi ya hadithi yenye mwisho mzuri wa furaha. Nadhani tunaweza kuona ongezeko kubwa la mashambulizi ya kijeshi ya Urusi mashariki, nadhani tunaweza kuona kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi ya Urusi kwenye mwambao wa pwani," afisa huyo aliwaambia waandishi wa habari.

Mkuu wa majeshi ya Ukraine alisema vikosi vya Urusi vimeongeza mashambulizi katika mstari wa mbele mashariki na walikuwa wakijaribu kufanya mashambulizi katika eneo la Kharkiv, kaskazini mwa shabaha yao kuu, Donbas.

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimekamata ghala kubwa la silaha katika eneo la Kharkiv. Pia iliripoti kuyapiga maeneo kadhaa katika mikoa ya Donetsk na Kharkiv siku ya Ijumaa.

Ukraine | Azovstal Iron Stahlwerk in Mariupol
Moshi ukifuka kutoka kiwanda cha chuma cha Azavtal wakati wa mzozo wa Urusi-Ukraine katika mji wa bandari ya kusini wa Mariupol, Ukraine Aprili 21, 2022.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Katika mji wa Kharkiv, makombora ya Urusi yalipiga soko kuu la Barabashovo. Idara ya huduma za kusafirisha wagonjwa ilisema kumekuwa na majeruhi lakini hakukuwa na maelezo ya kina bado. Ukumbi wa harusi na jengo la makazi pia vilipigwa.

Uhalifu wa kivita

Mjini Geneva, ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema kuna ushahidi unaoongezeka wa uhalifu wa kivita wa Urusi nchini Ukraine, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya makombora ya kiholela na mauaji ya kinyeme cha sheria. Ilisema Ukraine pia inaonekana ilitumia silaha zenye athari za kiholela.

Urusi inakanusha kuwalenga raia na kusema, bila ushahidi, kwamba dalili za ukatili uliofanywa na wanajeshi wake zilighushiwa. Ukraine hapo awali ilisema itawaadhibu wanajeshi wowote watakaobainika kufanya uhalifu wa kivita. Serikali haikujibu mara moja matamshi ya ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

Urusi ilisema siku ya Alhamisi kwamba imeshinda pambano kubwa zaidi la vita - vita vya Mariupol, bandari kuu ya Donbas, baada ya mzingiro wa karibu miezi miwili.

Rais Vladimir Putin alisema jeshi halitajaribu kuwatoa maelfu ya wanajeshi wa Ukraine ambao bado wamejichimbia kwenye kiwanda kikubwa ya chuma mjini Mariupol lakini wangewazuia ndani. Siku ya Ijumaa wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema kuwa wamesalia "kuzuiliwa salama".

Washington ilitupilia mbali tangazo la Urusi.

"Bado tathmini yetu inaonyesha kwamba Mariupol inagombaniwa, kwamba haijachukuliwa na Warusi na kwamba bado kuna upinzani mkali wa Ukraine," Msemaji wa Pentagon John Kirby aliiambia CNN.

Soma pia: Ukraine yatoa wito wa mazungumzo kuinusuru Mariupol

Katika sehemu inayoshikiliwa na Urusi ya mji huo, bunduki zilikuwa zimenyamaza kwa kiasi kikubwa wakaazi walioonekana wameduwaa waliingia mitaani siku ya Alhamisi ambako walikutana na majengo yayoungua na magari yaliyoharibika. Baadhi walibeba masanduku.

Maxer, kampuni ya kibiashara ya satelaiti, ilismea picha zilizopigwa kutokea angani zinaonesha makaburi mapya ya halaiki yaliochimbwa nje ya mji wa Mariupol.

Ukraine inakadiria kuwa mamia kwa maelfu ya raia wameuawa katika mji huo wakati wa mashambulizi ya Urusi na mzingiro na inasema raia 100,000 bado wako huko na wanahitaji kuondolewa kikamilifu.

Jamaa wa wakaazi wa Mariupol waliofia mabaya zaidi. Sofia Telehina alisema bibi yake alikuwa akilia mfululizo walipozungumza mara ya mwisho kwa simu na kusema kila kitu kiliripuriwa na kusambaratisha. "Tangu wakati huo sijaweza kumpata tena."

'Kubomoa kila kitu'

Katika mji wa Zaporizhzhia, ambako wakaazi 79 wa Mariupol wamewasili katika msafara wa kwanza wa mabasi ulioruhusiwa na Urusi kuondoka kwenda maeneo mengine ya Ukraine, Valentyna Andrushenko alizuwia machozi wakati akikukmbuka masaibu ya chini ya mzingiro.

Soma pia:Vita vya Ukraine vyautikisa uchumi wa dunia - IMF

"Walikuwa (Warusi) wanatupiga mabomu kuanzia siku ya kwanza. Walibomoa kila kitu," alisema akiulezea mji huo.

Moscow inasema imewapeleka wakaazi 140,000 wa Mariupol nchini Usuri. Kyiv inasema wengi wao walipelekwa kwa laazima katika kile kinachoweza kuwa uhalifu wa kivita.

Wa-Ukraine waapa kutetea maeneo yao

Katika hotuba yake ya usiku wa manane, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alisema Urusi ilikuwa inafanya kila inachoweza "kuzungumzia juu ya alau baadhi ya ushindi" baada ya kushindwa kuukamata mji mkuu wa Kyiv.

"Wanaahirisha tu kisichoepukika - wakati ambapo wavamizi watalaazimika kuondoka nchini mwetu, ikiwemo kutoka Mariupol, mji ambao unaendelea kuipinga Urusi bila kujali wanachokisema wakaliaji," Zelenskiy alisema.

Minnekayev, Jenerali wa Urusi, alisema wazungumzaji wa Kirusi walikuwa wanakandamizwa huko Transdnistria, ambayo ni sehemu inayokaliwa na Urusi ya Moldova kwenye mpaka wa kusini-magharibi wa Ukraine. Moldova na viongozi wa Magharibi wanasema hii siyo kweli.

Soma pia: Ukraine yaapa kutosalimu amri Mariupol

Moscow ilitoa sababu za hatua yake ya kuitwaa kimabavu rasi ya Crimea mwaka 2014 na kuwaunga mkono waasi wanaotaka kujitenga katika mkoa wa Donbas. Ukraine inasema inahofia Moscow inajaribu kuandaa kura bandia za uhuru katika maeneo yake ya kusini kama ilivyofanya mashariki na Crimea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ataizuru Moscow siku ya Jumanne kujadili njia za kurejesha haraka amani nchini Ukraine, alisema msemaji wake, na kuongeza kuwa Guterres huenda akaizuru pia Kyiv.

Chanzo: RTRE