1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, mkutano wa kilele wa Ukraine umefikia malengo yake?

17 Juni 2024

Mkutano wa kilele wa amani wa Ukraine uliofanyika nchini Uswisi mwishoni mwa Juma, ulihitimishwa na matokeo tofauti, kwani mataifa 80 pekee kati ya 93 yaliyoshiriki ndiyo yaliyodhinisha tamko la mwisho siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/4h9xv
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia mkutano huo
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy akihutubia mkutano huo Picha: Sean Kilpatrick/Zumapress/IMAGO

Kulingana na orodha iliyochapishwa na wenyeji wa Uswisi, nchi sita kutoka kundi la mataifa 20 yanayoongoza kiuchumi duniani ambayo ni Brazil, Mexico, Saudi Arabia, Afrika Kusini, India na Indonesia hayakuunga mkono tamko hilo la pamoja.

Yaliyozingatiwa kwenye tamko hilo lenye zaidi ya kurasa mbili, ni pamoja na tishio la matumizi ya silaha za nyuklia, wito wa kurejeshwa kwa watoto wa Ukraine waliohamishwa kinyume cha sheria, kuhakikisha bila vikwazo mauzo ya nafaka za Ukraine, haja ya mazungumzo na Urusi ili kufikiwa mkataba wa kudumu wa amani.

Soma pia: Mkutano wa kilele wa Ukraine waanza Uswisi lakini huenda ukashindwa kuitenga Urusi

Armenia, Bahrain, Thailand, Libya, Umoja wa Falme za Kiarabu, Colombia na Vatican pia hazikuunga mkono tamko hilo huko Bürgenstock nchini Usiwsi. Mataifa ya  Brazil, India, Afrika Kusini na UAE wamedhihirisha uungwaji wao mkono kwa Urusi kutokana na uwepo wao katika kinachojulikana kama muungano wa BRICS na kudhihirisha dhamira yao ya kudumisha uhusiano wa kirafiki na Urusi licha ya uvamizi wake nchini Ukraine mnamo Februari mwaka 2022.

Viongozi mbalimbali wa dunia wakishiriki mkutano huo wa kilele wa amani wa Ukraine nchini Uswisi
Viongozi mbalimbali wa dunia wakishiriki mkutano huo wa kilele wa amani wa Ukraine nchini UswisiPicha: Michael Buholzer/REUTERS

Rasimu ya tamko hilo la mwisho ilizingatia hali halisi ya baadhi ya mataifa kuwa na mahusiano ya karibu na Urusi na ndiyo maana haikulaani moja kwa moja uvamizi wa Moscow wala kuhimiza ijiondowe nchini Ukraine. Badala yake, imekumbushia tu kipengele muhimu katika  Mkataba wa Umoja wa Mataifa  kuhusu umuhimu wa kuheshimu uhuru na uhalali wa maeneo ya mataifa yote ikiwemo Ukraine, kwa kuzingatia mipaka inayotambuliwa kimataifa.

Mitazamo tofauti kuhusu matokeo ya mkutano huo

Rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky  ameelezea kuhusu uwezekano wa kufanyika mnamo miezi kadhaa ijayo mkutano wa pili wa kilele, huku nchi kadhaa zikionyesha nia ya kuwa mwenyeji wa tukio hilo ambalo Saudi Arabia inapewa kipaumbele. Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesisitiza kuwa ushiriki wa Urusi katika mkutano huo utahitaji kwanza kuthibitisha iwapo vitendo vya Moscow vinaendana na uheshimishwaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kuanzia kulia: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Chile Gabriel Boric na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau
Kuanzia kulia: Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Rais wa Chile Gabriel Boric na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano huo nchini Uswisi.Picha: Sean Kilpatrick/ZUMA Press/IMAGO

Kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba, mkutano huo hata hivyo uliwezesha kufikiwa kwa hatua muhimu na kwamba mchakato ulioanzishwa unaashiria kuwa wapo kwenye njia sahihi. Lakini Kwa upande wa Ikulu ya Kremlin, mkutano huo ulikuwa sawa na sifuri na ulidhihirisha wazi kuwa mazungumzo yoyote kuhusu mzozo wa Ukraine yasiyoishirikisha Urusi hayawezi kuwa na matokeo chanya.

Soma pia: Viongozi wa dunia waunga mkono suluhisho la amani kwa mzozo wa Ukraine

Rais wa Uswisi Viola Amherd alizingatia mitazamo tofauti katika mkutano huo lakini akasisitiza kuwa ni tukio la kwanza lililowakusanya viongozi wa ngazi za juu kwenye mazungumzo ya amani, na kwamba tukio hilo lililenga kuanzisha mchakato wa muda mrefu wa amani ambao utaijumuisha pia  Urusi.

Mkutano huo wa siku mbili nchini Uswisi ambao Urusi haikualikwa ulikuwa pia ni jaribio la nchi za Magharibi kuzihusisha nchi nyingine kutoka Amerika ya Kusini, Asia na Afrika katika juhudi za amani chini ya sheria ya kimataifa.

(Chanzo: DPAE)