Janga la Njaa na matumaini yanayochomoza Somalia Magazetini
10 Machi 2017Tunaanzia katika pembe ya Afrika ambako magazeti mengi yamezungumzia wiki hii kuhusu janga la ukame na kitisho cha watu kufa kwa njaa. "Maonyo yote yamepuuzwa", na "balaa lililotoa ishara" ni miongoni mwa vichwa vya maneno vya ripoti za magazeti ya Ujerumani kuhusu janga la njaa na ukame unaopiga katika nchi nyingi za Afrika Mashariki. Mamilioni kadhaa ya watu wanakabiliwa na hatari ya ukosefu wa chakula katika eneo hilo. Gazeti la die Tageszeitung linazungumzia onyo la Umoja wa mataifa uliotahadharisha Somalia na mataifa mengineyo ya mashariki mwa Afrika yanaelekea katika janga kubwa la ukosefu wa chakula. Janga hilo lakini dalili zake zimeanza kujitokeza tangu zamani. Ulimwengu unaufumbia macho mzozo wa njaa nchini Somalia amenukuliwa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guteress akisema alipokuwa ziarani nchini Somalia.
Mabadiliko ya tabia nchi yaathiri shughuli za kilimo Afrika
Die Tageszeitung linanukuu ripoti ya Umoja wa Mataifa inayosema watu wasiopungua milioni 23 hawatakuwa na chakula cha kutosha Afrika Mashariki kutokana na balaa la ukame. Nchi zinazokumbwa na mizozo ya mtutu wa bunduki ndizo zinazoathirika zaidi, mfano wa Somalia na Sudan Kusini ambako gazeti linasema watu milioni nne na laki tisa wanakabiliwa na kitisho cha njaa na laki moja wanakaribia kufa kwa njaa. Ukame unapiga pia katika nchi ambayo kawaida ina rutuba ya Burundi linamaliza kuandika gazeti la die Tageszeitung linaloyataja madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kuwa mojawapo ya sababu za hali hiyo.
Matumaini ya wasomali
Mapambazuko yachomoza Mogadishu ndio kichwa cha maneno cha gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linalozungumzia kuhusu viongozi wepya wa Somalia. Somalia sasa itakuwa ikiongozwa na mnorway na mmarekani , viongozi wawili wenye uraia wa nchi mbili na ambao fikra za kikoo hawanazo hata kidogo.
Uongozi mpya wa Somalia si wa kawaida, linaandika gazeti la Frankfurter Allgemeine, rais Mohammed Abdullahi Mohammed na waziri mkuu Hassan Ali Khaire hawalingani hata kidogo na mifano ya viongozi wa awali wa nchi hiyo inayozoroteshwa na kudidimizwa kutokana na fikra za kikoo na rushwa. Viongozi hao wawili lakini, mbali na kuwa raia wa Somalia wana uraia wa nchi nyengine jambo ambalo viongozi wa koo haliwafurahishi hata kidogo. Abdullahi Mohammed ana uraia wa Marekani na waziri mkuu Ali Khaire ni raia wa Norway. Wote wawili wamekulia katika mfumo wa demokrasia na kwa namna hiyo mbali kabisa na desturi na mila za koo za nchi yao ya asili.
Rais mpya wa Somalia awasihi wasomali wawe na subira
Frankfurter Allgemeine linazungumzia sifa anazojivunia rais Abdullahi Mohammed mjini Mogadishu, tangu alipokuwa waziri mkuu kati ya mwaka 2010 hadi 2011. Katika kipindi cha miezi minane tu madarakani alifanikiwa kupunguza idadi ya mawaziri ,kupunguza ziara ambazo si muhimu nchi za nje, na kuhakikisha watumishi wa serikali na wanajeshi wanalipwa wakati unapowadia ili kupunguza angalao sababu mojawapo ya rushwa nchini humo. Kwa upande wake waziri mkuu Hassan Ali Khaire ingawa ni mgeni katika majukwaa ya kisiasa nchini Somalia, lakini ana sifa za utu na imani. Kati ya mwaka 2011 hadi 2014 alikuwa akiongoza tawi la shirika la misaada ya kiutu la baraza la wakimbizi la serikali ya Norway nchini Somalia, kabla ya kuteuliwa mwaka 2015 kuwa mkurugenzi wa kampuni la mafuta na gesi la Uingereza-la Soma. Matumaini ni makubwa mjini Mogadishu tangu Abdullahi Mohammed alipochaguliwa kuwa rais, kwa namna ambayo amelazimika kuingilia kati na kuwatanabahisha wasomali, alipotoa hotuba yake ya kwanza rasmi na kusema miaka minne haitoshi kumaliza uharibifu wa miaka 30.
Kesi dhidi ya wanaharakati wanaoikosoa serikali Zimbabwe yafutwa
Mada yetu ya mwisho katika ukurasa wa Afrika katika magazeti ya Ujeruimani wiki hii inatufikisha Zimbabwe ambako gazeti la die Tageszeitung linaandika kuhusu kufutiliwa mbali kesi dhidi ya vuguvugu la waandamanaji 65 wanaoikosoa serikali , na kuwaachia huru, wengi wao wakiwa vijana. Wanaharakati hao waliteremka majiani julai 4 mwaka jana , wakitia moto mipira ya magari na kuweka vizuwizi majiani, wakilalamika dhidi ya rushwa na ufisadi. Walikamatwa na kutiwa ndani kwa madai ya kuhatarisha usalama na kuvunja nidhamu. Jaji Victoria Mashamba ameikataa hoja hiyo akisema polisi haijawahoji vizuri watuhumiwa, na hakuna mashahidi waliotajwa. Kesi imefutwa linamaliza kuandika die Tageszeitung lililokumbusha Mugabe, mwenye umri wa miaka 93, anapanga kugombea tena wadhifa huo uchaguzi utakapoitishwa mwakani.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/PRESSER/ALL/presse
Mhariri: Iddi Ssessanga