1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Italia yapiga kura kuchagua bunge jipya

25 Septemba 2022

Italia inafanya uchaguzi Jumapili ambao unatarajiwa kurejesha muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia madarakani tangu Vita Vikuu vya Pili vya Ulimwengu.

https://p.dw.com/p/4HJR0
Wahl in Italien - Stimmabgabe
Picha: Alessando Di Marco/Asna/picture alliance

Aidha, kwa mara ya kwanza mwanamke anatarajiwa kushika wadhifa wa Waziri Mkuu wa nchini humo.

Vituo vya upigaji kura vilifunguliwa asubuhi na vitafungwa saa tatu usiku.

Japo matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa Jumapili usiku, kulingana na sheria ya uchaguzi nchini humo, itachukua saa kadhaa kabla ya idadi kamili ya viti ambavyo vyama vimeshinda kujulikana.

Kulingana na kura ya maoni iliyochapishwa wiki mbili zilizopita, muungano wa mrengo wa kulia unaoongozwa na Giorgia Meloni wa chama cha Brothers, unatarajiwa kushinda kwenye uchaguzi huo.

Hata hivyo hayo yanaweza kubadilika. Katika wiki mbili zilizopita, kumekuwa na madai kwamba katika siku za hivi karibuni, uungwaji mkono wa vuguvugu la Nyota 5 (5-Star), la siasa za mrengo wa kushoto na ambacho ndicho chama kikubwa zaidi Italia tangu mwaka 2018, umekuwa ukiongezeka.

Uungwaji mkono wa vuguvugu la Nyota Tano

Uungwaji mkono wa hivi karibuni wa vuguvugu hilo la Nyota Tano huweza kuathiri nafasi za muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia kushinda viti vingi kwenye baraza la bunge na baraza la seneti, na unaweza kuhujumu zaidi mchakato wa kuunda serikali.

Hata kama kutakuwa na matokeo ya wazi, huenda serikali mpya isianze kazi hadi mwisho wa Oktoba, ikizingatiwa bunge litaanza vikao Oktoba 13.

Giorgia Meloni wa chama cha Brothers, anapigiwa upatu kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Italia endapo muungano wake utashinda.
Giorgia Meloni wa chama cha Brothers, anapigiwa upatu kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa Italia endapo muungano wake utashinda.Picha: Alessandro Garofalo/LaPresse/AP/picture alliance

Meloni ambaye ni kiongozi wa muungano wa vyama vya siasa za mrengo wa kulia, anatazamiwa kuwa mgombea wa nafasi ya waziri mkuu. Muungano huo unajumuisha pia chama cha League chake Matteo Salvini na chama cha Forza Italia chake Silvio Berlusconi.

Berlusconi akanusha kula njama kumuangusha Draghi

Ushirikiano huo unatarajiwa kumpa Meloni mwenye umri wa miaka 45 kura zaidi, tofauti na hali ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2018, ambapo chama chake kilipata 4% pekee ya kura.

Uchaguzi huo wa kwanza kufanyika katika msimu wa mapukutiko nchini Italia kwa Zaidi ya karne, ulisababishwa na mivutano ndani ya chama iliyosababisha iliyokuwa serikali ya Umoja wa kitaifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu Mario Draghi kuanguka mwezi Julai.

Hali ya misukosuko ya kisiasa ya Italia

Italia imekuwa na historia ya misukosuko ya kisiasa. Serikali mpya itakayoundwa itakuwa ya 68 tangu mwaka 1946. Waziri Mkuu mpya ajaye atatarajiwa kukumbwa na changamoto si haba, hususan ongezeko la bei ya nishati.

Wakuu wa Umoja wa Ulaya wanaojizatiti kukuza ushirikiano wao, hasa baada ya Urusi kuivamia Ukraine, wana wasiwasi kwamba Italia itakuwa mshirika asiyetabirika kuliko ilivyokuwa chini ya uongozi wa Draghi.

Matokeo ya uchaguzi huo yatatizamwa kwa hofu na nchi za Ulaya Pamoja na masoko ya kifedha.
Matokeo ya uchaguzi huo yatatizamwa kwa hofu na nchi za Ulaya Pamoja na masoko ya kifedha.Picha: Ettore Ferrarie/picture alliance

Kwa masoko ya fedha, kuna hofu ya mara kwa mara kuhusu uwezo wa Italia kudhibiti madeni yake yanayofikia takriban 150% ya jumla ya mapato yake.

Meloni amekuwa akipuuza madai dhidi ya chama chake kuwa na mizizi ya kifashisti mambo leo. Badala yake anakiangazia kama chama cha kihafidhina. Ameahidi kuunga mkono sera za Magharibi kuhusu Ukraine na kutochukua hatua za hatari wakati huu ambapo uchumi umeathiriwa na kupanda kwa bei ya bidhaa.

Hata hivyo kuna dalili za migawanyiko kati ya Meloni na washirika wake kuhusu sera ya kigeni.

Kiongozi wa chama cha League, Salvini amekosoa athari ya kupanda kwa bei ya nishati kwa Waitalia akielekeza sehemu ya lawama kwa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Urusi. Berlusconi alizusha ghadhabu kwenye kampeni alipoonekana kumtetea Vladimir Putin.

(Rtre)

Tafsiri: John Juma

Mhariri: Sylvia Mwehozi