1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yakosolewa kwa kushambulia kituo cha UNIFIL

11 Oktoba 2024

Israel imekabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya vikosi vyake kushambulia kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL).

https://p.dw.com/p/4lfcH
Kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) katika mji wa Naqoura.
Kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) katika mji wa Naqoura.Picha: AFP

Wanajeshi wa Israel wamekishambulia kwa risasi hivi leo kituo kikuu cha uchunguzi cha kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL kilichopo katika mji wa Naqoura kusini mwa Lebanon na kuwajeruhi watu wawili. Hayo yameelezwa na chanzo cha Umoja wa Mataifa ambacho kimeongeza pia kuwa vikosi vya Israel viliingia kinyume cha sheria kwenye eneo jingine linalosimamiwa na UNIFIL na ambalo lilishambuliwa pia jana Alhamisi.

China kupitia msemaji wa wizara ya mambo ya nje Mao Ning imeelezea wasiwasi wake mkubwa na kulaani vikali mashambulizi ya Israel dhidi ya ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa. Uturuki pia ililaani mashambulizi hayo yanayowalenga walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL , na kusisitiza kuwa serikali mjini Ankara itaendelea kuunga mkono operesheni kama hizo za kulinda amani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: William Volcov/ZUMA Press Wire/picture alliance

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari pembezoni mwa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti ili kuepusha vita kamili nchini Lebanon, akisema kuwa kuongezeka kwa migogoro katika eneo la  Mashariki ya Kati ni kitisho kikubwa kwa usalama wa dunia. Aidha, Guterres amelaani pia mashambulizi ya Israel dhidi ya kituo cha Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa askari wa kulinda amani ni lazima walindwe. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema amani inahitajika.

"Amani inahitajika zaidi sasa kuliko hapo awali, unaposhuhudia mateso makubwa ya watu wa Gaza, ambayo sasa yameenea hadi nchini Lebanon, bila kusahau Ukraine, Sudan, Myanmar na kwengineko. Nathubutu kuwaambia kwamba kiwango cha vifo na uharibifu huko Gaza ni mambo ambayo hayawezi kulinganishwa na hali nyingine yoyote ambayo nimeishuhudia tangu niwe Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa."

Mashambulizi yaendelea Lebanon

Uharibifu mjini Beirut uliosababishwa na mashambulizi ya Israel
Uharibifu mjini Beirut uliosababishwa na mashambulizi ya Israel (10.10.2024)Picha: Hassan Fneich/AFP

Huku hayo yakiarifiwa, watu 22 wameuawa na wengine zaidi ya 100 wamejeruhiwa mjini Beirut kufuatia mashambulizi ya Israel huku chanzo kilicho karibu na kundi la Hezbollah kikisema kuwa mashambulizi hayo yalikuwa yakimlenga mkuu wa usalama wa kundi hilo Wafiq Safa.

Soma pia: Marekani yaionya Israel kuhusu uharibifu Lebanon

Kwa upande mwingine Iran imesema haitasita kuchukua hatua kali zaidi ikiwa Israel italipiza kisasi mashambulizi yake ya makombora ya hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amesema leo Ijumaa kuwa Tehran imejiandaa kikamilifu kukabiliana na uchokozi wowote wa ziada. Kauli hiyo imetolewa baada ya Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant kusema kuwa Israel itaishambulia Iran kwa njia sahihi, ya kushangaza na itakayosababisha vifo.

(Vyanzo: AP, Reuters, DPAE, AFP)