1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaanzisha operesheni kali Ukingo wa Magharibi

28 Agosti 2024

Jeshi la Israel limeilenga miji minne katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu, na kuanzisha operesheni mpya sawia na vita vyake vya zaidi ya miezi kumi katika Ukanda wa Gaza. Limeitaja kuwa operesheni ya ugaidi.

https://p.dw.com/p/4k0Sd
Ukingo wa Magharibi | Operesheni ya Kijeshi ya Israel.
Wapalestina wakitathmini uharibifu kwenye gari wakati wa operesheni ya vikosi vya Israel karibu na Jenin, Ukingo wa Magharibi, Agosti 28, 2024.Picha: Ali Sawafta/REUTERS

Maafisa wa afya wa Palestina wanasema vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina tisa katika uvamizi kwenye Ukingo wa Magharibi, wakati jeshi likionekana kuanzisha operesheni kwenye miji kadhaa kwa mara moja, huku duru zikiarifu kuwa operesheni hiyo huenda ikadumu kwa siku kadhaa.

Wizara ya Afya ya Palestina imesema wanaume wawili waliuawa katika mji wa Jenin na saba mjini Tuba mapema leo. Wizara hiyo imewatambua wawili waliouawa mjini Jenin kuwa Qassam Muhammad Jabarin mwenye umri wa miaka 25, na Asema Walid Balout mwenye umri wa miaka 39.

Jeshi la Israel limethibitisha kufanya operesheni mjini Jenin na Tulkarem, mji mwingine wa Ukingo wa Magharibi, likiitaja operesheni hiyo kuwa ya kupambana na ugaidi. Waziri wa mambo ya nje Israel Katz, alisema jeshi lilikuwa "linafanya operesheni kwa nguvu kamili tangu usiku uliopita", katika juhudi za "kuvunja miundombinu ya ugaidi wa Irana."

Soma pia: Hamas yaikosoa Israel kuhusu uwepo wake wa kijeshi mpakani

Katika chapisho la mtandao wa kijamii wa X, aliituhumu Iran, ambayo ni hasimu mkuu wa Israel katika kanda hiyo, kutaka "kuanzisha safu ya mashariki dhidi ya Israel" kwa msingi ya "ruwaza" ya Gaza na Lebanon, ambako inaziunga mkono Hamas na Hezbollah mtawalia.

Uvamizi wa vikosi ya Israel Jenin
Israel imewakamata maelfu ya Wapalestina pia katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza.Picha: Leo Correa/AP Photo/picture alliance

"Laazima tushughulikia kitisho hiki kwa nguvu sawa inayotumiwa dhidi ya miundombinu ya kigaidi Gaza, ikiwemo uhamishaji w amuda wa wakaazi na hatua zozote muhimu," alisema. "Hivi ni vita, na laazima tuvishinde."

Makundi wa wapiganaji wa Kipalestina yamesema yalikuwa yanarushiana risasi na jeshi la Israel. Gavana wa Jenin, Kamal Abu-al-Rub, alisema kupitia redio ya Palestina kwamba vikosi vya Israel vilikuwa vimeuzingira mji huo, na kuzuwia njia za kuingia na kutoka hospitali, na kuvunja miundombinu kwenye kambi ya wakimbizi.

Ukingo wa Magharibi wazidi kulengwa na Israel

Makabiliano na jeshi la Israel yameongezeka pakubwa katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza. Maelfu ya Wapalestina wametiwa nguvuni katika operesheni za kijeshi, na wasiopungua 637 wameuawa kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya ya Palestina. Wengi wao wanaripotiwa kuwa wapiganaji, lakini wengine ni vijana wanaorusha tu mawe na raia wasiohusika.

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas alikatisha ziara yake nchini Saudi Arabia kurejea Ukingo wa Magharibi Jumatano, kufuatia operesheni hizo za Israel, lilisema shirika rasmi za habari la Palestina, Wafa.

Soma pia: Netanyahu ataacha urathi gani baada ya vita vya Gaza?

"Abbas alikatisha ziara ya Saudi Arabia na kurejea nchini wake Jumatatu, kufuatilia matukio ya karibuni katika muktadha wa uchokozi wa Israel Kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi," lilisema shirika la Wafa.

Rais wa Mamlaka ya Wapalestian Mahmoud Abbas
Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas amekatisha ziara yake nchini Saudi Arabia kufuatia operesheni ya Israel Ukingo wa Magharibi.Picha: Adem Altan/AFP/Getty Images

Operesheni hii ya karibuni imekuja siku mbili baada ya Israel kusema ilifanya shambulizi la ndege dhidi ya Ukingo wa Magharibi, ambalo Mamlaka ya Wapalestina ilisema liliuwa watu watano.

Jeshi la Israel limethibitisha vifo hivyo vitano Jumatano, na kusema shambulizi hilo lilipiga kile lilichokiita kituo kinachotumiwa na magaidi kufanya shughuli za ugaidi na kuwadhuru wanajeshi wanaoendesha operesheni katika eneo hilo.

Kundi la Islamic Jihad, ambalo linashirikiana na Hamas katika Ukanda wa Gaza na lina uwepo mkubwa kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, limetoa taarifa mapema leo likilaani kile lilichokiita vita vya wazi vya Israel.

Kwa upande wake, Hamas ambayo umaarufu wake umeongezeka sana katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita vya Gaza, ilikariri wito wake jana jioni kwa Wapalestina katika eneo hilo kuasi.

Wapatanishi wakutana Doha kujadili usitishaji vita Gaza

Taarifa yake ilikuja kama jibu kwa matamshi yaliotolewa na waziri wa uslaama wa Israel mwenye msimamo mkali Itamar Ben Gvir, aliesema wiki iliyopita kwamba angejenga sinagogi kwenye eneo la Msikiti wa Al-Aqsa iwapo angeweza.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Ben Gvir, ambaye mwenyewe ni mlowezi, ametoa wito wa wazi wazi wa kunyakuliwa kwa Ukingo wa Magharibi.

Soma pia:Hezbollah yavurumisha makombora dhidi ya Israel 

Shambulio la Hamas na Oktoba 7, lilisababisha vifo vya watu 1,199, wengi wao raia, kwa mujibu wa takwimu za serikali ya Israel. Kampeni ya kujibu ya Israel tangu wakati huo imeua watu wasiopungua 40,534 Gaza, kulingana na wizara ya afya ya ukanda huo. Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema wengi wao ni wanawake na watoto.

Wakati huo huo, duru zimearifu kuwa wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar wanakutana hii leo mjini Doha, kwa ajili ya mazungumzo ya ngazi ya kitaalamu kuhusu mpango wa kusitisha vita Gaza, bila hata hivyo kutoa ufafanuzi zaidi.

Chanzo chenye ufahamu juu ya mazungumzo ya kusitisha vita Gaza limesema Jumatano kuwa ujumbe wa Israel uliwasili Doha kwa majadiliano ya "ngazi ya kitaalamu" na wapatanishi kuhusu mapatano na ubadilishanaji wa mateka na wafungwa.