1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na wanamgambo wa kipalestina wasitisha mapigano

Admin.WagnerD14 Novemba 2019

Israel na wanamgambo wa itikadi kali wa kiislamu wa Islamic Jihad wameafikiana kusitisha mapigano kati yao ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 34 na kusimamisha shughuli mbalimbali katika maeneo kadhaa ya Israel. 

https://p.dw.com/p/3T1Di
Israel - Palästina - Konflikt l Raketenangriffe auf Israel
Picha: picture alliance/AA/A. Amra

Sasa ni afueni kwa raia wa kawaida katika ukanda wa Gaza na maeneo ya Israel baada ya Israel na wanamgambo wa Islamic Jihad kuafikiana kuweka silaha chini na kusitisha mapigano kati yao.

Msemaji wa wanamgambo hao Musab al-Berim amesema kuwa maafikiano hayo yameanza kutekelezwa kuanzia leo alfajiri huku naye msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Avichay Adraee akiandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa oparesheni yao Gaza imekamilika.

Yamkini Misri imekuwa na mchango mkubwa katika upatanishi huo.

Baada ya maafikiano hayo, sasa baadhi ya vikwazo vilivyowekwa kwa baadhi ya wakaazi wa kusini mwa Israel vimeondolewa huku hali ya kawaida ikirudi katika barabara za eneo la Pwani ya Palestina.

Mapigano yatatiza shughuli za kawaida

Gaza Streifen Baby bei der Ruine eines palästinensischen Hauses
Picha: Reuters/I. Abu Mustafa

Hali hiyo iliathiri masomo Israel huku shule zikifungwa na watu kulazimika kusalia majumbani.

Huyu ni mkaazi wa Gaza akieleza kuhusu athari ya mapigano hayo.

"Tunataka amani, hatutaki vita. Mimi nafanya kazi, na kwa sababu ya vita kwa wakati huu sifanyi kazi."

Al-Berim ameongeza kuwa kusitishwa kwa mapigano hayo kulitokana na mahitaji yaliotolewa na wanamgambo hao ikiwemo kuitaka Israel kukomesha mashambulizi yao yaliolenga viongozi wakuu wa kundi hilo.

Msemaji wa jeshi la Israel hakuthibitisha moja kwa moja iwapo mahitaji ya wanamgambo wa Islamic Jihad yalizingatiwa katika maelewano yao ya kusitisha mapigano.

Hata hivyo, katika hali ya kutilia shaka maelewano hayo, waziri wa mambo ya nje wa Israel Yisrael Katz  amesema kuwa wataendelea kuwashambulia wanamgambo ambao amewataja kama hatari kwa usalama licha ya maafikiano hayo ya kusitisha mapigano.

Kwanini kulizuka mapigano?

Gazastreifen | Trümmer eines Hauses nach israelischem Raketenangriff
Picha: Reuters/I. Abu Mustafa

Mapigano yalizuka upya baada ya Israel kufanya shambulizi la anga mapema wiki hii lililomuua kiongozi wa wanamgambo wa Islamic Jihad Bahaa Abu el-Atta, mkewe na kuwajeruhiwa watoto wake wawili.

Punde tu baada ya kuuawa kwa Bahaa Abu el-Atta, wanamgambo hao walijibu mashambulizi hayo ya angani kwa kurusha makombora 400 yaliyofika hadi eneo la Tel Aviv kama njia ya kulipiza kisasi.

Jeshi la Israel lilisema kuwa Abu el-Atta ndiye aliyeongoza mashambulizi dhidi ya Israel na amekuwa kiungo muhimu katika kupanga mashambulizi ya makombora na yale ya ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya Israel.

Aidha kujitenga kwa kundi la wanamgambo la Hamas ambalo ni kubwa na lenye nguvu zaidi kuliko kundi la Islamic Jihad katika maafikiano hayo ya kusitisha mapigano, kumetafsiriwa kuwa sio mwisho wa vita kati ya Israel na makundi ya wanamgambo.