1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na UAE zasaini makubaliano ya biashara huru

31 Mei 2022

Kulingana na upande wa Israel, makubaliano hayo yanaondoa asilimia 96 ya ushuru wa bidhaa zote zinazouzwa kati yao.

https://p.dw.com/p/4C69P
VAE und Israel unterzeichnen Kooperationsvertrag in Dubai
Picha: WAM/AFP

Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu, leo zimesaini makubaliano ya kwanza ya biashara huru baina yao, ikiwa ni muendelezo wa  kukuza uhusiano wa kidiplomasia kati yao waliorejesha mwaka 2020 na kusimamiwa na Marekani. 

Kulingana na upande wa Israel, makubaliano hayo yanaondoa asilimia 96 ya ushuru wa bidhaa zote zinazouzwa kati yao.

Balozi wa Israel katika Umoja wa Falme za Kiarabu, taifa lenye utajiri wa mafuta, Amir Hayek, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter ‘Mabruk' neno la Kiarabu lenye maana ya hongera.

Bennet akutana na mrithi wa ufalme wa Abu Dhabi Mohammed bin Zayed Al Nahyan

Biashara kati ya Israel na UAE kutanuka zaidi

Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Israel, Mohamed Al Khaja, aliyapongeza makubaliano hayo na kuyataja kuwa ‘mafanikio ambayo hayajawahi kutokea.

Uhusiano wa Israel. UAE, Morocco na Bahrain watimiza mwaka

Amesema biashara katika nchi hizo mbili zitanufaika kwa kuweza kufikia masoko kwa haraka na kodi za chini, wakati nchi hizo zikiendelea pia kuimarisha biashara, kubuni nafasi za ajira, kukuza taaluma mpya na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Kulingana na takwimu za Israel, mwaka uliopita, biashara kati ya Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu ilitinga dola milioni 900.

Rais wa baraza la kibiashara kati ya Israel na taifa hilo la kifalme Dorian Barak, alibashiri kwamba biashara kati ya nchi hizo mbili itaongezeka zaidi.

Kwenye taarifa aliandika, " Thamani ya biashara kati ya Israel na Umoja wa Falme itapita dola bilioni mbili mwaka 2022, na itafikia dola bilioni tano katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema kwenye taarifa.

Kampuni za Israel zawekeza Dubai

Kampuni nyingi za Israel zimeanza kuwekeza mjini Dubai. Barak amesema ifikapo mwisho wa mwaka huu, takriban kampuni 1,000 za Israel zitakuwa zikifanya kazi ndani au kupitia Umoja wa Falme za Kiarabu zikilenga masoko ya Asia Kusini na  Mashariki ya Mbali.

Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi 8katikati), Waziri Mkuu wa israel Naftal Bennet (Kulia) na Mfalme wa Umoja wa falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed, wakati wa mkutano wa kilele kati yao mjini Sharm al-Sheikh nchini Misri mnamo Machi 22, 2022.
Rais wa Misri Abdel Fattah Al-Sisi 8katikati), Waziri Mkuu wa israel Naftal Bennet (Kulia) na Mfalme wa Umoja wa falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed, wakati wa mkutano wa kilele kati yao mjini Sharm al-Sheikh nchini Misri mnamo Machi 22, 2022.Picha: Embassy of Israel in Egypt/AA/picture alliance

Makubaliano kati ya nchi hizo mbili kurejesha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 2020, chini ya mpango wa Marekani kwa jina Abrahamic Accord, yalisababisha pia Israel kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na Bahrain na vilevile Morocco.

Umoja wa Falme za kiarabu ilikuwa nchi ya kwanza kurejesha uhusiano wa diplomasia na Israel, na taifa pekee la tatu la kiarabu kufanya hivyo baada ya Misri na Jordan.

Mazungumzo ya biashara huru kati yao yalianza mwezi Novemba na yalikamilika baada ya duru nne za majadiliano. Duru ya hivi karibuni Zaidi ilifanyika Misri kati ya Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett na Sheikh Mohammed bin Zayed Al-Nahyan, mtawala wa muda mrefu ambaye alichukua hatamu za urais mwezi huu kufuatia kifo cha kaka yake, Sheikh Khalifa.

(AFPE)