1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yamfukuza Balozi wa Sweden baada ya Quran "kunajisiwa"

21 Julai 2023

Iraq imemfukuza balozi wa Sweden nchini humo na kutangaza dhamira ya kupunguza ushirikiano na taifa hilo la Scandinavia baada ya waandamanaji kukikanyaga hadharani kitabu kitukufu kwa waislamu, Quran, mjini Stockholm.

https://p.dw.com/p/4UCs8
Nakala ya Quran
Nakala ya QuranPicha: Pascal Deloche/Godong/picture-alliance/dpa

Amri ya kufukuzwa kwa mwanadiplomasia huyo imetolewa na waziri mkuu wa Iraq Mohammde Shia al-Sudani aliyesema imechochewa na "mwenendo wa serikali ya Sweden wa kutoa vibali kila wakati kwa maandamano yanayojumuishwa kuchomwa Quran na kunajisiwa alama nyingine tukufu za dini hiyo."

Serikali ya nchi hiyo pia imesema imemrejesha nyumbani mkuu wa kituo chake cha ubalozi nchini Sweden na imefutilia mbali leseni ya kazi kwa kampuni kubwa ya simu ya Sweden ya Ericsson.

Utawala mjini Baghdad vilevile umeiarifu serikali ya Sweden kuwa kujirudia kwa tukio linalohusisha kuchomwa au kunajisiwa kwa Quran kwenye ardhi ya Sweden kutatatiza kabisa mahusiano baina ya pande hizo mbili.

Hapo jana mhamiaji mmoja kutoka Iraqi anayeishi nchini Sweden alipewa ruhusu ya kufanya maandamano ambapo alishuhudiwa akikanyaga nakala ya kitabu cha Quran.

Mwanaume huyo aliruhusiwa kufanya hivyo mbele ya ubalozi wa Iraq mjini Stockholm akiwa na dhamira ya kuchoma nakala ya kitabu hicho.

Kwenye tukio hilo mhamiaji huyo na waandamanaji wengine walikipiga mateke, kukikanyaga  na kukiharibu kitabu waliyechosema ni Quran lakini waliondoka eneo la maandamano bila kukichoma moto. Hata hivyo mnamo mwezi Juni mwanaume huyo wa Kiiraqi alichoma nakala ya Quran mbele ya msikiti kwenye mji huo mkuu wa Sweden.

Mataifa ya kiarabu na yenye waislamu wengi yachachamaa 

Kisa hicho cha jana Alhamisi na kile cha mwezi Juni vyote vilizusha hasira na ukosoaji mkali kutoka mataifa ya kiarabu na yale yenye waislamu wengi duniani.

Pakistan: Maandamano ya kuipinga Sweden
Matukio ya kuchomwa au kunajisiwa kwa Quran yamezusha ukosoaji kutoka mataifa yenye waumini wengine waislamu ikiwemo maandamano kama ilivyofanyika huko Pakistan.Picha: Raja Imran/Pacific Press/picture alliance

Kisa cha kukanyagwa Quran hapo jana kimetia kiwingu mahusiano ya Sweden na mataifa yenye waislamu wengi. Wizara ya mambo ya kigeni ya Iran ilimwita balozi wa Sweden mjini Tehran na kulalamika kwa matamshi makali dhidi ya kunajisiwa kwa Quran huku Uturuki ikisema matendo yaliyoshuhudiwa mjini Stockholm "yanakarahisha". Jordan, Saudi Arabia na Qatar nazo zimelalamika kuhusu tukio hilo.

Huko Lebabon mkuu wa kundi la wanamgambo wenye nguvu la Hezbollah, Sayyed Hassan Nasrallah aliyatolea mwito mataifa ya kiarabu na yale ya kiislamu kuchukua mkondo sawa na wa Iraq wa kuwafukuza mabalozi wote wa Sweden kutoka kwenye nchi zao na kuwarejesha nyumbani wawakilishi wao wa kidiplomasia mjini Stockholm.

Je, uhuru wa maoni na kujieleza hauna mipaka nchini Sweden? 

Schweden erlaubt Verbrennung der Torah
Picha: Caisa Rasmussen/TT News Agency/AP Photo/picture alliance

Usiku wa kuamkia jana waandamanaji nchi Iraq waliuvamia na kuchoma moto sehemu ya ubalozi wa Sweden mjini Baghdad kulaani ruhusa iliyotolewa kwa mwanaume huyo kufanya kile waandamanaji walikitaja kuwa "kuinajisi" Quran.

Hakuna mtu aliyedhurika kwenye uvamizi huo lakini Sweden ilisema Iraq ilishindwa kutoa ulinzi unaofaa kwenye majengo ya ubalozi wake. Marekani, Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Ulaya zimelaani uvamizi huo wa majengo ya ubalozi wa Sweden.

Katika miaka ya karibuni Sweden imeshuhudia matukio kadhaa ya kuchomwa moto hadharani kwa kitabu cha Quran megni yakifaynwa na wanaharakati wa mrengo mkali wa kulia na wale wanaoupinga Uislamu.

Mapema mwaka huu polisi ya nchi hiyo ilizuia maombi kadhaa ya maandamano ambayo yangejumuisha uchomaji wa Quran lakini mahakama zilitengua maamuzi hayo zikisema matendo ya aina hiyo yanalindwa na sheria za uhuru wa kujieleza nchini humo.