Iran,Russia,Uturuki kuweka msimamo wa pamoja Syria
3 Aprili 2018Marais wa mataifa hayo matatu , Vladimir Putin , Recep Tayyip Erdogan , na Hassan Rouhani wa Iran , ambao kwa muda mrefu walionekana kuwa mahasimu wa kimkoa badala ya washirika wa kimkakati, watakutana leo mjini Ankara kwa mkutano wao wa pili wa kilele kuhusu Syria katika hatua ya kuonesha umoja wao.
Mkutano huu , ambao unafuatia mkutano wa kwanza wa kilele baina ya viongozi hao mjini Sochi Novemba mwaka jana, unakuja wakati Uturuki ikiwania kupata sauti kubwa baada ya kuazisha mashambulizi dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi ndani ya Syria.
Rais wa Marekani Donald Trump ameashiria kwamba nchi yake itakuwa inajiondoa "hivi karibuni" kutoka Syria , katika hatua ambay itaimarisha ushawishi wa Uturuki , Urusi na Iran nchi ambazo zimekuwa na majeshi yao ndani ya nchi hiyo.
Sinan Ulgen , mwenyekiti wa kituo cha sra za mchanganuo wa mawazo katika masuala ya kiuchumi na sera za mambo ya kigeni cha mjini Istanbul, amesema mataifa hayo matatu sasa yamekuwa wadhibiti wakuu ndani ya Syria.
Ulgen aliliambia shirika la habari la AFP kwamba mataifa hayo matatu yamekuwa "mataifa yenye nguvu kimkoa ambayo yako tayari kuwekeza rasilmali za kijeshi kushawishi matokeo ya mzozo huo."
Mataifa hayo matatu mwaka jana yalianzisha mchakato wa kuleta amani sambamba na mazungumzo yanayoongozwa na Umoja wa mataifa mjini Geneva. Mazungumzo hayo , ambayo yanafanyika Astana, yamefanyika mara kadhaa bila ya kupata suluhisho.
Mchakato wa Astana
"Mchakato wa mjini Astana ni chombo ambacho Uturuki , Urusi na Iran , vinakiangalia kuweza kudhibiti vita na kupata maslahi yao mbali mbali," amesema Elizabeth Teoman , mchambuzi wa Uturuki katika taasisi iliyoko mjini Washington katika mitaala ya vita (ISW).
Urusi ina uwezo mkubwa wa nguvu za angani nchini Syria wakati Iran ina vikosi vya jeshi lake la ardhini , kwa kiasi fulani kwa kutumia makundi ya wanamgambo ambayo ni pamoja na wapiganaji wa kigeni.
Lakini Erdogan ameongeza ushawishi wa Uturuki kwa kuazisha mwezi Januari mashambulizi kuukamata ardhi kutoka kwa vikosi vya wanamgambo wa ulinzi wa umma vya Wakurdi vya YPG.
Mashambulizi hayo tayari yamefanikisha kukamatwa kwa eneo la zamani wa YPG la Afrin na Erdogan ametishia mara kadhaa kuendeleza msukumo wake kuelekea zaidi upande wa mashariki.
"Erdogan ni mshirika dhaifu kwa misingi wa majeshi ya ardhini na udhibiti wa anga. Lakini amejenga uwiano na kuthibitisha kwamba anaweza kujenga uwezekano ndani ya nchi hiyo," amesema Teoman.
Lakini wachambuzi bado wana shaka juu ya uwezekano wa muda mrefu wa utendaji wa muungano huo kati ya mataifa hayo makubwa matatu ambayo yametumia historia yao kubwa ya vita na kupigana vikumbo kuwania ushawishi katika eneo hilo la bahari nyeusi. Kinadharia bado wanaendelea kuwa katika pande zinazotofautiana katika mzozo huo , ambapo Urusi na Iran zikitoa usaidizi wa kijeshi kwa utawala wa Syria wa rais Bashar al-Assad lakini Uturuki mara kwa mara ikitoa wito Assad aondolewe.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman