1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaonya kuhusu kuishambulia miundombinu ya Israel

4 Oktoba 2024

Naibu kamanda wa kikosi cha ulinzi wa mapinduzi ya Iran IRGC amesema kikosi chake kitalenga miundombinu ya nishati ya Israel iwapo patatokea vita kamili kati ya mataifa hayo mawili.

https://p.dw.com/p/4lQV5
Iran, Teheran | Fadavi
Naibu Kamanda wa kikosi cha IRGC cha Iran Ali Fadavi Picha: Rouzbeh Fouladi/ZUMA Press/picture alliance

Naibu Kamanda wa kikosi hicho Ali Fadavi ametaja mitambo ya mafuta kama maeneo yanayotarajiwa kulengwa, Iwapo Israel itaamua kulipiza kisasi, hatua ya Iran kuishambulia kwa makombora zaidi ya 180. Iran ilisema ilichukua hatua hiyo kuiadhibu Israel kwa mashambulizi yake inayoendelea kufanya nchini Lebanon na Gaza, na mauaji pia ya kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh na mwenzake wa Hezbolla Hassan Narallah.

Hamas na Hezbollah ni makundi ya wanamgambo yanayoungwa mkono na Iran. Mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya makundi hayo yaliwajeruhi pia makamanda wa ngazi ya juu wa kikosi cha kimapinduzi cha Iran IRGC. Kiongozi wa juu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, alitoa hotuba yake ya nandra kwa wananchi wakati wa sala ya Ijumaa akisema mataifa ya Kiislamu yana adui mmoja huku akitetea hatua ya nchi hiyo ya kuishambulia Israel. Khamenei alionya kuwa nchi yake haitorudi kwenye upinzani wake dhidi ya utawala wa Israel.

Huku hayo yakiarifiwa jeshi la Israel limesema limefanikiwa kuwauwa wapiganaji 250 wa kundi la Hezbollah ndani ya siku nne zilizopita, baada ya kuanzisha operesheni za ardhini Kusini mwa Lebanon zilizolenga maeneo 2000 ya wanamgambo hao ikiwemo majengo na maghala yao ya silaha. Katika taarifa yake, Jeshi hilo limesema miongoni idadi hiyo ya waliouwawa 21 ni makamanda wakuu wa kundi hilo.

Hospitali kadhaa zasitisha operesheni zake Lebanon

Beirut
Mashambulizi ya Israel yaendelea kurindima mjini Beirut Picha: Ugur Can/ABACA/IMAGO

Wakati huo huo hospitali tatu nchini Lebanon ikiwemo moja ilioko nje kidogo ya mji wa Beirut zimetangaza kusimamisha operesheni zao kufuatia mashambulizi ya Israel yanayoendelea. Hospitali ya  Sainte Therese,  Mais al-Jabal na hospitali ya serikali ya Marjayoun zote zimesimamisha kazi zake zikisema mashambulizi ya Israel yanawalenga kwa maksudi na kulenga pia magari ya kubebea wagonjwa.  Hata hivyo Israel imesema inawalenga wanamgambo wa Hezbollah kwa nia ya kulifanya eneo la Kaskazini mwa Israel salama ili wakaazi waliopoteza makaazi yao huko waweze kurejea nyumbani. Kando na hayo Waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati ameitolea mwito Jumuiya ya Kimataifa  kuishinikiza Israel kuruhusu makundi ya kutoa misaada kuingia katika maeneo yaliyoathirika na vita kuwasaidia majeruhi baada ya zaidi ya wahudumu 40 wa afya kuuwawa katika mashambulizi hayo.

Haya yote yanatokea wakati Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Abbas Araghchi akiwa mjini Beirut kwa mazungumzo na viongozi wa Lebanon. Wataalamu wanasema huenda mazungumzo hayo yakawa yalituwama katika kumtafuta mrithi wa Hassan Narallah Kiongozi wa Hezbollah aliyeuwawa wiki iliyopita. Baada ya mazungmzo yake na spika wa bunge Nabih Berri Araghchi pia alitoa onyo kali kwa Israel kwamba ikisubutu kuishambulia itajibiwa na mashambulizi makali zaidi.

Kwengineko ndege moja ya kijeshi ya Uholanzi iliwasili mjini Beirut kuwachukua raia wake kwa kuhofia hali kuwa mbaya zaidi. Serikali ya Japan pia imetangaza kuwaondoa raia wake waliofikishwa Jordan leo asubuhi. Uingereza kwa upande wake imesema raia wake wanaendelea kuhamishwa kutoka Lebanon baada ya kufanikiwa kuwaondoa wengine 150.

afp/ap/reuters