1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IOC na Japan zadhamiria kufanikisha Olimpiki licha ya corona

16 Novemba 2020

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC Thomas Bach na Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga wamekubaliana leo kuifanikisha michezo ya Olimpiki licha ya janga la Covid-19.

https://p.dw.com/p/3lMzO
Japan Olympia Tokio 2020 Yoshihide Suga und Thomas Bach
Picha: Kazuhiro Nogi/AP Photo/picture alliance

Bach aliyewasili Tokyo jana kwa ziara ya siku nne, amefanya mazungumzo na Suga kwa mara ya kwanza tangu Suga alipoingia madarakani miezi miwili iliyopita. Wamejadili hatua za kuandaa michezo hiyo katika majira ya kiangazi mwaka ujao chini ya mazingira salama licha ya kuibuka wimbi jipya la corona Ulaya na Marekani. Suga amesisitiza kuwa amedhamiria kuiandaa michezo hiyo, ambayo iliahirishwa mwezi Machi kwa mwaka mmoja hadi Julai 23, 2021.

Bach amesema washiriki wa Olimpiki na mashabiki watakaowasili kwa ajili ya michezo hiyo huenda wakahitajika kuwa wamepata chanjo ili kuulinda umma wa Japan. "Tumeona matukio mengi ya michezo kote duniani ambayo yameandaliwa kwa ufanisi na kuwapa watu matumaini na uhakika. Wanamichezo, maafisa na makocha wote wanahitaji kuamini kuwa wanashiriki na kushindana katika mazingira salama, na kuwa kanuni zile zile na vizuizi vinatumika kwa wote."

Gavana wa Tokyo Yuriko Koike amesema maafisa wanapambana kuweka hatua mwafaka za kupambana na Covid-19 mjini humo kabla ya tamasha kuanza.

Afp, ap, reuters, dpa