1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
AfyaIndia

India yaweka vizuizi baada ya kirusi cha Nipah kuuwa watu 2

14 Septemba 2023

Serikali nchini India imeweka vizuizi baada ya watu wawili kufariki dunia kwa kirusi cha Nipah, huku zaidi ya watu 700 wakifanyiwa vipimo kubaini ikiwa wameambukizwa kirusi hicho ambacho bado hakina chanjo.

https://p.dw.com/p/4WK3D
Watu wakiwa wamevalia mavazi ya kujizuia kuambukizwa wakibeba mwili wa aliefariki kwa virusi vya Nipah India
Watu wakiwa wamevalia mavazi ya kujizuia kuambukizwa wakibeba mwili wa aliefariki kwa virusi vya NipahPicha: Shijith. K/AP Photo/picture alliance

Wahudumu wa afya 153 wako chini ya uangalizi baada ya kujihusisha na watu waliopata maambukizi hayo.

India imezuia mikusanyiko ya watu na kufunga baadhi ya shule katika jimbo la kusini la Kerala baada ya watu wawili kufariki kwa ugonjwa unaosababishwa na kirusi cha  Nipah.

Virusi hivyo vinavyotajwa kutoka kwapopo au nguruwe husababisha homa kali, kutapika, kushindwa kupumua na hata kusababisha ugonjwa wa kupooza.

Watu watatu wamegundulika kuambukizwa virusi hivyo huku zaidi ya watu 700 wakiwemo wafanyakazi wa afya 153 ambao waliwahudumia watu hao walioambukizwa wakitengwa kwa ajili ya uangalizi  zaidi.

Soma pia:Wakati msimu wa kiangazi unamalizika, maambukizi ya virusi vya corona yanaongozeka. Je pana hatari ya janga la corona kurudi tena nchini Ujerumani?

Wakati watu hao waliofanyiwa vipimo wakisubiria majibu ya vipimo vyao, mamlaka katika eneo hilo la kusini mwa India inatarajiwa kufanya vipimo kwa watu wengi zaidi ili kubaini ukubwa na kasi ya kusambaa kwa virusi hivyo ambavyo hadi sasa vimeleta taharuki miongoni mwa watu nchini India.

Kiongozi Mkuu wa jimbo la Karela,  Pinarayi Vijayan amewaamuru watu katika jimbo hilo hasa katika wilaya ya Kozhikode kuepuka mikusanyiko isiyo na ulazima kwa angalau siku 10 ili kupunguza kasi ya maambukizi.

 WHO: Yazungumzia virusi hivyo hatari

Shirika la Afya duniani WHO linaeleza kwamba virusi hivi hatari vya Nipah vinaambukizwa kutoka kwa wanyama kama nguruwe na popo na kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Dalili za awali zinajidhihirisha baada ya siku nne hadi kumi na nne baada ya maambukizi.

Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Ghebreyesus
Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Ghebreyesus Picha: Lian Yi/Xinhua/picture alliance

WHO inasema wakati mwingine inaweza kuchukua muda mrefu wa hadi siku 45.

 Mwaka 2018, watu wasiopungua 17 walikufa baada ya kuambukizwa na virusi hivyo huko Kerala nchini India.

Soma pia:WHO kujadili kitisho cha UVIKO-19

Jimbo jirani la Tamil Nadu limetangaza kuwa wasafiri wanaotokea katika jimbo la Kerala watalazimika kufanyiwa vipimo vya afya na wale watakaobainika kuwa na maambukizi watalazimika kujitenga kwa muda.

 Virusi hivyo vilitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998 baada ya kusambaa miongoni mwa wafugaji wa nguruwe nchini Malaysia.

Huko India, mlipuko wa kwanza wa Nipah uliripotiwa katika jimbo la West Bengal mnamo 2001.

Shirika la Afya Duniani WHO limeorodhesha virusi vya Nipah kama ugonjwa hatari zaidi kwa umma.

Imeinywa kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuwa janga kubwa kwa kuwa bado hakuna njia za kutosha za kuweza kuukabili.