India yapeleka chombo karibu na uso wa mwezi
23 Agosti 2023India leo imekuwa taifa la kwanzakupeleka chombo karibu na upande wa kusini kabisa wa uso wa mwezi. Tukio hilo ni ushindi wa kihistoria kwa taifa hilo lenye idadi kubwa kabisa ya watu ulimwenguni na mpango wake kabambe wa utafiti wa anga za mbali.
Chombo cha Chandrayaan-3 kilitua mwezini majira ya saa kumi na mbili jioni saa za India huku waongozaji safari hiyo wakishangilia na kukumbatiana na wafanyakazi wenzao.
Kutua kwa chombo hicho kumejiri siku chache tu baada ya chombo cha Urusi kuanguka katika eneo hilo hilo na miaka minne tangu jaribio la awali la India kushindwa katika dakika za mwisho.
Waziri Mkuu Narendra Modi alionesha tabasamu kubwa na kupeperusha bendera ya India kwenye matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ili kutangaza mafanikio ya ujumbe huo akisema ni ushindi uliokwenda mbali ya mipaka ya nchi yake.
Ilikichukua chombo hicho mwezi mmoja kufika mwezini, na sasa kitafanya utafiti kwenye uso wa mwezi kwa wiki mbili na kurusha data kwenye sayari ya Dunia.