1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo "Mediterania" huenda ikaongezeka

30 Machi 2020

Mashirika ya uokoaji katika bahari ya mediterenia yana wasiwasi kwamba idadi ya wahamiaji wanaofariki wakati wa kuvuka bahari hiyo wakielekea Ulaya huenda ikaongezeka.

https://p.dw.com/p/3aDGO
Griechenland Insel Lesbos Migranten erreichen Küste
Picha: picture-alliance/dpa/AP/M. Varaklas

"Kwa bahati mbaya idadi ya vifo itaongezeka” anasema Frederic Penard wa shirika la SOS Mediteranee, shirika linalojihusisha na shughuli za kuwaokoa watu waliokwama katika bahari ya Mediterenia. Katika mahojiano na DW, Penard analalamika kwamba kwa sasa hakuna kabisa meli za kuwaokoa watu katika pwani ya Libya. Anakumbuka kwamba operesheni ya Umoja wa Ulaya iitwayo operesheni Sophia iliwaokoa maelfu ya watu kati ya mwaka 2015 na 2018.

Kisiwa cha Lampedusa nchini Italia na msaada kwa wahamiaji

Lakini katika kipindi cha majira ya joto mwaka 2018, Umoja wa Ulaya ulibadilisha sera yake kutokana na shinikizo kutoka kwa serikali ya Italia iliokuwa inaelemea siasa za mrengo wa kulia. Sera hiyo ilihakikisha kwamba operesheni Sophia haina meli za kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha wiki chache tu hiyo basi haikuweza kutekeleza majukumu yake.

Serikali za Italia, Hungary na Austria zilikuwa zinaunga mkono kusitishwa kwa biashara ya silaha lakini pia walikuwa wanataka kuwazuia maelfu ya watu kutoka Afrika na Asia ambao walikuwa wanaingia Ulaya kutokana na operesheni hiyo. Kwa hiyo, Italia na serikali zengine za Ulaya zikaifutilia mbali operesheni Sophia, jambo lililopingwa na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.

DW-Reportage-Reise Miodrag Soric | Rettungsschiff Ocean Viking | 2. Tagebucheintrag
Mmoja ya wahamiaji wanaookolewa kwenye bahari ya Mediterania.Picha: DW/M. Soric

Hassiba Hadj Sahrouai ni mshauri wa haki za binadamu katika shirika la madaktari wasio na mipaka na katika mahojiano na DW anasema, ni wazi kwamba Umoja wa Ulaya umekataa kabisa wazo la kuokoa maisha. Sahrouai amekosoa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na kikosi cha ulinzi wa pwani ya Libya akidai ni wazi kwamba kikosi hicho cha ulinzi wa pwani ya Libya kinahusika katika ukiukaji wa haki za binadamu.

Uhusiano kati ya mashirika ya kutoa misaada na uongozi wa kijeshi wa operesheni Sophia umekuwa mzuri siku zote. Mashirika yote, lile la madaktari wasio na mipaka na SOS Mediteranee yamethibitisha kuwa yalifanya kazi vyema na operesheni Sophia mwaka 2015 na 2016. Sahrouai anasema waliokoa maisha ya watu kwa pamoja ila tangu wakati huo ushirikiano huo umekuwa ukipungua hasa baada ya Umoja wa Ulaya kuwataka wahamiaji wasalie Libya.

Waziri wa nchi za kigeni wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani Heiko Maas, amekuwa akijadiliana na mawaziri wenzake wa Ulaya kuhusiana na operesheni "Irini” kwa miezi sasa. Operesheni Irini inalenga kuichukua nafasi ya operesheni Sophia. Mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya yalikubaliana Alhamis kuhusiana na jukumu la operesheni hiyo. Lakini waziri Maas pia aliweka wazi kwamba lengo la operesheni hiyo ni kuangalia iwapo biashara ya silaha ingali inaendelea.