1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAEA yatakiwa kufanyiwa mageuzi.

Charles Hilary20 Aprili 2006

Wakiwa wanaelewa kitisho kikubwa kinaweza kuletwa na teknolojia ya nuklia kwa mazingira pamoja na mashaka yanayozingira mizozo ya kisiasa juu ya suala hilo,baadhi ya wanasiasa wa nchi za Ulaya,wameshauri wakati umefika kwa Umoja wa Mataifa kuachana na mipango ya kuikuza teknolojia ya nuklia,ikiwa ni njia pekee kwa dunia kupambana na mahitaji yanayokuwa ya nishati.

https://p.dw.com/p/CBIw
Mohammed ElBaradei,Mkurugenzi Mkuu wa IAEA.
Mohammed ElBaradei,Mkurugenzi Mkuu wa IAEA.Picha: dpa

Viongozi wa mataifa ya Ulaya ambao waliwahi kuzitumikia nchi zao katika nyadhifa za uwaziri wa mazingira,wamemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Kofi Annan,kufanyia mageuzi mamlaka ya Shirika la Kimataifa la Udhibiti wa Teknolojia ya Nishati ya Nuklia,IAEA,ambayo wanayaona yamepitwa na wakati na pia yanakanganya.

Shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1957,likiwa na makao yake mjini Vienna,limepewa jukumu la kukagua vinu vya nuklia duniani kote,ili kuhakikisha teknolojia hiyo haitumiki kwa malengo ya kijeshi.Lakini wamsema wanasiasa hao katika hali inayotia mashaka,mamlaka yake yanapindukia katika kutafuta,kuhakikisha usalama na amani kwa teknolojia ya nguvu za nuklia.

Kwa mujibu wa Satu Hassi,mbunge katika Bunge la Umoja wa Ulaya na waziri wa zamani wa mazingira wa Finland,ameeleza katika taarifa yake,kwamba jukumu la kusambaa kwa silaha za nuklia,linaonekana kukua kwa haraka.

Hassi pamoja na wanasiasa wengine,wanaona IAEA haina meno ya kuzuia usambaaji wa silaha za nuklia na wakati huo huo,pia ikijishughulisha kuyashawishi mataifa kujitahidi kuwa na teknolojia ya nishati ya nuklia,ambayo pia hutengeneza nyenzo kwa ajili ya mabomu.

Ni hivi majuzi tu Hassi na mwenzake Dominique Voynet,waziri wa zamani wa mazingira wa Ufaransa,walimwandikia barua Bwana Annan,wakimuarifu kuwa mzozo wa sasa wa mipango ya nuklia ya Iran,ambao umechukua nafasi kubwa miongoni mwa jumuia ya kimataifa,ni sawa na ugutusho uliokuja wakati muafaka wa majukumu ya kukanganya ya IAEA.

Kwa wakati huu IAEA imejiingiza zaidi katika jitahada za kupata uhakikisho,iwapo Iran inafuata mkataba wa kuzuia kuenea kwa Nuklia,ikiwa ni matokeo ya shinikizo la kimataifa.

Marekani na baadhi ya mataifa ya Ulaya,yamekuwa yakiishutumu Iran kwa kujaribu kutengeneza silaha za nuklia,huku Iran yenyewe ikidai kuwa mipango yake ya nuklia ina lengo la kutoa nishati ya umeme tu.

Wakielezea hatari inayoweza kuletwa na teknolojia ya nuklia,mawaziri hao wa zamani wa mazingira wa nchi za Ulaya,wamesema wanalitaka shirika la IAEA kusimamisha mara moja majukumu yake ya kuwa madalali wa teknolojia hiyo na pia wakati huo huo kuwa msimamizi kwa biashara ya viwanda,ambayo imefanya gharama ya umeme duniani kuwa ghali kwa teknolojia ya nuklia,ambayo kuwepo kwake kunaweza kuwa kwa miaka mingi ijayo.

Wamedai wanasiasa hao kuwa kwa sasa nishati ya nuklia sio muhimu tena,kwani dunia inavyanzo vingi mbadala vya teknolojia ya nishati inayopatikana kwa urahisi na inayohakikisha usalama,usafi na unafuu wa gharama.

Mahitaji ya kutaka kuwepo na mabadiliko katika majukumu ya IAEA,yamekuja wakati muafaka ambapo maadhimisho ya miaka 20 tokea mkasa wa ajali ya kinu cha Chernobly yakiwa yanakaribia.Inakumbukwa tarehe 26 mwezi kama huu mwaka 1986,mripuko katika kinu hicho cha nuklia cha Chernobly huko Ukraine,umeleta maafa makubwa na athari zake zinaendelea kuonekana hadi wakati huu.Tukio hilo,linahesabika ni ajali mbaya ya mitambo ya nuklia kuwahi kutokea duniani.

Watu wanaofikia kati ya 4,000 na 9,000 bado wanatazamiwa watakufa kutokana na maradhi ya kansa yaliyosababishwa na ajali ya Chernobly.