1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW yaishutumu Somaliland kukandamiza uhuru wa kutoa maoni

Isaac Gamba
9 Mei 2018

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mfululizo wa visa vya kuwafungulia mashitaka watu wanaokosoa serikali ni ukandamizaji uhuru wa kutoa maoni.

https://p.dw.com/p/2xQG7
Markt in Somalia
Picha: picture alliance/Africa 24 Media/Tim Freccia

Katika taarifa yake hii leo Human Rights Watch imesema hivi karibuni kiongozi mmoja wa kijamii katika jimbo hilo alishitakiwa na hatimaye April 26,  kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani katika hukumu iliyosomwa kwa muda usio zidi nusu sasa.

Katika kipindi cha mwezi mmoja tu uliopita serikali ya jimbo la Somaliland iliwafungulia mashitaka watu watatu kwa kutumia vifungu vya kisheria vinavyokandamiza uhuru wa kutoa maoni.  Human Rights Watch imesema sheria hizi zinatumika kuwabana wale wanaokosoa sera za serikali ya jimbo hilo pamoja na wale wanaokosoa utendaji wa baadhi ya maafisa wa serikali.

Laetitia Bader mtafiti mwandamizi wa shirika hilo kanda ya Afrika amesema nafasi ya jamii kuikosoa serikali katika jimbo hilo kuhusiana na masula yenye utata inazidi kupungua siku hadi siku na kuongeza hali hii ni kinyume cha haki za binadamu na inaonekana kuichafua taswira ya serikali ya jimbo hilo.

Human Rights  Watch imesema mashitaka ya namna hii yanatoa picha kuwa maafisa wa kiserikali katika jimbo la Somaliland hawatavumilia kauli zozote zinazoonekana kutengeneza mazingira ya kutaka serikali ya jimbo hilo ijitathimini katika utendaji wake.

Jimbo la Somaliland lilijitangazia uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991 lakini hadi sasa halijatambulika kimataifa.

Mivutano yaripotiwa kuongezeka

Journalistentraining in Somaliland Juli 2017
Waandishi wa habari katika jimbo la Somaliland wakiwajibikaPicha: DW Akademie/H. Weithöner

Tangu Januari mwaka huu mivutano kati ya jimbo la Somaliland na jimbo lenye mamlaka yake ya  ndani la Puntland kwenye eneo la mpaka linalozozaniwa katika mkoa wa Sool imeongezeka huku jimbo la Somaliland likilazimika kupeleka vikosi vyake na kudhibiti vituo vya kijeshi katika mji wa Tukaraq.

April 19, maafisa wa polisi walimtia mbaroni kiongozi mmoja wa kijadi Boqol Osman Mohamud anayefahamika kama Buur Madow baada ya kiongozi huyo kutoa mwito  kwa serikali ya jimbo la Somaliland na Puntland  kuondoa vikosi vyao katika eneo la mpaka unaozozaniwa la Sool hatua iliyofuatiwa na kiongozi huyo wa kijadi kufunguliwa mashitaka na hatimaye kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano gerezani na rufaa yake kupinga hukumu hiyo iliyokuwa ikitarajiwa kusikilizwa  Mei 8,  inaonekana kucheleweshwa.

Licha ya mashitaka hayo waandishi wa habari nao pia wamekuwa wakinyanyaswa pamoja na kushitakiwa wakiwemo waandishi wa habari wanne ambao wameshitakiwa  wakituhumiwa kusambaza propaganda dhidi ya serikali  kwa kutumia vifungu vya kisheria vya aina hiyo tangu wakati alipoapishwa rais mpya wa jimbo hilo.

Human Rigths Watch imetoa mwito kwa bunge la Somaliland  kufuta haraka sheria  zinazozuia uhuru wa kutoa maoni katika masuala ya kisiasa na ukosoaji dhidi ya maafisa wa serikali.

Mwandishi: Isaac Gamba- Human Rights Watch

Mhariri :Yusuf Saumu