1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Vikosi vya Ethiopia vilitekeleza uhalifu Amhara

Hawa Bihoga
3 Julai 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema vikosi vya Ethiopia vimetekeleza mashambulizi makubwa kama "uhalifu wa kivita" dhidi ya sekta ya afya katika eneo la Amhara

https://p.dw.com/p/4hoDe
Ethiopia, Amhara | Wanajeshi wakiwa katika doria
Wanajeshi wa Ethiopia wakifanya doria katika moja ya mji eneo la AmharaPicha: Minasse Wondimu Hailu/AA/picture alliance / AA

Ripoti ya shirika hilo yenye kurasa 66 ambayo iliwahoji  watu takriabn 58 wakiwemo waathirika na mashuhuda, imerekodi visa vya mashambulizi yaliofanywa na vikosi vya serikali na wanamgambo wa Fano dhidi ya wahudumu wa sekta ya afya, vituo vya afya pamoja na miundombinu ya usafirishaji katika miji takriban 13.

Sehemu ya ripoti hiyo ya Human Rights Watch ilisema kwamba askari waliwapiga, kuwakamata kiholela wahudumu wa afya kwa kuwapa huduma majeruhi na wagonjwa ikiwa ni pamoja na wapiganaji wanaodaiwa kuwa wa Fano.

Aidha ripoti hiyo imeongeza kuwa vikosi hivyo vilishambulia magari ya wagonjwa kinyume na sheria na kuzuia hospitali kutoa huduma.

Soma pia:HRW yataka UN kulichunguza jeshi la Ethiopia kwa mauaji

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu limesema kuwa sheria ya kimataifa ya kibinaadamu inatoa ulinzi kwa miundombinu katika sekta ya afya, wahudumu, wagonjwa, lakini sheria hiyo imekiukwa kwa kiwango kikubwa wakati wa makabiliano na kuleta hofu miongoni mwa waathirika katika mzozo huo.

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika Laetitia Bader amesema kwamba vikosi vya serikali ya Ethiopia viliendesha operesheni zake kwa "kupuuza maisha ya raia" kwa kushambulia miundombinu muhimu ikiwa ni pamoja na vituo vya afya.

Shirika hilo limesema mashirika ya misaada ya kiutu yalitatizika katika kuendesha shughuli zake katika eneo hilo lenye wakaazi takriban milioni 23, huku wafanyakazi wa mashirika hayo wakiwa ni miongoni mwa walengwa kwani tangu kuzuka kwa mapigano wafanyakazi tisa tayari wameuwawa ikiwa ni pamoja na vifo vinne kwa mwaka huu.

Kubinywa haki za binadamu Amhara

Ripoti hiyo imeendelea kuonesha kwamba kumekuwa na vikwazo vikali hata kwa vyombo vya habari kuripoti yale yanayoendelea katika eneo hilo la Amhara, katika wakati ambao Tume ya Wataalam wa Umoja wa Mataifa inayochunguza ukatili nchini Ethiopia ilimalizi kazi yake mwezi Oktoba, na kusababisha ufuatiliaji mdogo wa ukiukaji wa haki nchini humo.

Ethiopia | Maandamano ya kupinga mapigano Amhara
Maandamano ya raia wa Ethiopia wanaopinga mapigano eneo la Amhara.Picha: Marcello Valeri/ZUMA/picture alliance

Ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema "vikosi vya Ethiopia na wanamgambo wa Fano wamehusika katika ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za binadamu, na kusababisha zaidi ya 2,000 kuuwawa na wengine kujeruhiwa katika eneo hilo la Amhara.

Soma pia:Wanajeshi wa serikali walaumiwa kuwauwa raia wasiopungua 45 katika jimbo la Amhara

Ghasia za Amhara zilizusha wasiwasi kuhusu utulivu wa Ethiopia, miezi kadhaa baada ya makubaliano ya amani kusainiwa mwezi Novemba 2022 ili kumaliza mzozo wa miaka miwili katika eneo jirani la Tigray.

Vikosi vya Amhara na wanamgambo wa Fano viliunga mkono wanajeshi wa Ethiopia wakati wa vita hivyo lakini vilijiengua baada ya Addis Ababa kutia saini mkataba wa amani mnamo 2022, na kuchochea hisia za usaliti kwa Amhara, ambao wana historia ya migogoro ya ardhi na eneo la Tigray.