HRW: Jeshi la Rwanda latumia mbinu za kikatili
10 Oktoba 2017Kulingana na ripoti ya shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch iliyotolewa leo (Oktoba 10) kuna visa zaidi ya 100 vya watu kuzuiwa na kuteswa kinyume na sheria katika vituo vya kijeshi vya Rwanda kati ya mwaka 2010 hadi mwaka jana.
Shirika hilo limesema madai ya kuteswa na wanajeshi huwa mara nyingi yanapuuzwa na majaji na waendesha mashitaka nchini humo wakati wafungwa wanapolalamika.
Afisa wa Human Rights Watch, Isa Sawyer, anasema wanajeshi wa Rwanda hutumia mateso wanapopenda.
Wengi wa waathirika wanazuiwa kwa tuhuma kuwa ni wanachama wa kundi la waasi wa Kihutu la FDLR lenye makao yake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wengine wanashukiwa kuwa na mafungamano na chama cha upinzani cha Rwanda National Congress (RNC) kilicho uhamishoni.