1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Iran awasili Saudi Arabia

17 Agosti 2023

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amewasili mjini Riyadh ikiwa ni ziara yake ya kwanza Saudi Arabia, tangu mataifa hayo mawili yalipoamua kuanzisha tena uhusiano wao mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/4VIsq
Mwanamfalme Faisal Bin Farhan wa Saudi Arabia akiwa pamoja na Hossein Amir-Abdollahian wa Iran
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Mwanamfalme Faisal Bin Farhan na mwenzake wa Iran Hossein Amir-Abdollahian Picha: AHMED YOSRI/REUTERS

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Iran Hossein Amir-Abdoll-ahian alisafiri kuelekea Riyadh kufuatia mualiko alioupata kutoka kwa Waziri mwenzake Mwanamfalme wa Saudi Arabia.

Wawili hao walikutana katika wizara ya mambo ya nje ya Saudia na baadae kuwa na mkutano na waandishi habari ambapo mwanamfalme Farhan, alisema taifa hilo linatumai rais wa Iran Ebrahim Raisi atakubali mualiko wa mwenzake Mfalme Salman bin Abdulaziz na kulitembelea taifa hilo hivi karibuni. 

Ujumbe wa Iran wazuru Saudia kusawazisha mahusiano

Ameongeza kuwa mabalozi wa mataifa hayo, wataanza rasmi majukumu yao baada ya balozi hizo kufungiliwa kufuatia nchi hizo kukubaliana kusitisha uhasama wao mwezi Machi na kufufua uhusiano wao. Ziara hiyo ya siku moja inalenga kujadili mambo kadhaa ikiwemo kuimarishwa kwa uhusiano wa mataifa hayo, masuala ya kikanda na mambo mengine muhimu ya kimataifa.

Bin Farhan aliitembelea Iran mwezi Juni, ziara ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa ndani ya miaka mingi na mwakilishi wa ngazi ya juu wa serikali hiyo ya Kisuni kwa eneo lililo na Washia walio wachache Iran.

Mahusiano mema kati ya mataifa hayo mawili huenda yakaleta faida kikanda

Waziri wa mabo ya nje wa Iran Hossein Amirabdollahian na mwenzake Mwanamfalme Faisal wa Saudia
Waziri wa amabo ya nchi za kigeni wa Iran Hossein Amirabdollahian akiwa na mwenzake wa Saudi Arabia Faisal Bin Farhan Al Saud wa Saudi Arabia baada ya kukubaliana kurejesha mahusiano ya mataifa hayo mawili Picha: Rouzbeh Fouladi/Zuma/Imago

Duru kadhaa za mazungumzo tayari zimefanyika miongoni mwa wawakilishi wa mataifa yote mawili nchini Iran, hasa juu ya masuala ya usalama. Hivi karibuni shirika la habari la kitaifa la Iran lilitangaza kuwa maafisa wa kijeshi wa nchi hizo mbili walikutana mjini Moscow, Urusi pembezoni mwa mkutano wa usalama uliofanyika huko.

Kurejea kwa uhusiano huu huenda kukasababisha kupigwa kwa hatua kubwa za kikanda hasa nchini Yemen ambako uungwaji mkono wa Iran na Saudi Arabia kwa pande zinazohasimiana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea huko, vilivyosababisha vifo vya maelfu ya watu pamoja na njaa.

Wasaudia wakutana na waasi wa Houthi kutafuta amani Yemen

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Iran na Saudi Arabia ulizidi kuingia doa kufuatia ubalozi wa Saudia nchini Iran kushambuliwa wakati wa maandamano ya kupinga kuuwawa kwa kiongozi wa kishia wa Iran Nimr al Nimr mwaka 2016.

Iran na Saudi Arabia zina historia ndefu ya uhusiano mbaya na ni mahasimu wa kikanda, lakini mwezi Machi majirani hao walitangaza nia yao ya kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia kama sehemu ya mapatano yaliyosimamiwa na China.

Chanzo: reuters/dpa