1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Historia ya wazo la mataifa mawili: Israel na Palestina

Daniel Gakuba
20 Mei 2021

Wakati mzozo ukiendelea baina ya Waisraeli na Wapalestina, suluhisho la mataifa mawili linatajwa tena kama muarobaini wa kumaliza uhasama baina ya jamii hizo mbili. Lakini je, wazo la suluhisho hilo lilianza lini?

https://p.dw.com/p/3tgL5
USA Israel-Palästina Abkommen 1993
Picha: picture-alliance/ZumaPress

Kwa mara ya mwanzo kabisa suluhisho la mataifa mawili kati ya Waisraeli na Wapalestina lilianzishwa na Tume ya Peel, ambayo iliundwa wakati wa utawala wa Uingereza katika nchi ambayo wakati huo iliitwa Palestina, kati ya mwaka 1922 na 1947. Mwaka 1937 tume hiyo ilipendekeza kuwa Palestina igawanywe katika mataifa mawili; la Wayahudi na la Wapalestina.

Pendekezo hilo lilifuatia mahojiano na mamia ya watu kutoka kila jamii, ambayo yalibainisha tofauti kubwa za kimtazamo baina yao. Tume ya Peel iligundua kuwa kila upande, Wayahudi na Waisraeli haukutaka kuishi pamoja na mwingine, na malengo yao ya utaifa yalikuwa hayatangamani hata kidogo.

Licha ya kuwekwa kabatini, pendekezo hilo laweka msingi wa fikra

Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kulishughulikia pendekezo hilo, lakini baadaye lilitumiwa kama msingi katika majaribio yoyote ya baadaye ya kuunda mataifa hayo mawili, ambayo yote yamefeli. Wakati taifa la Israel lilipotangazwa mwaka 1947, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililifikiria pia pendekezo hilo, lakini mataifa ya Kiarabu yalilikataa katakata, kwa sababu hayakutaka kusikia chochote kuhusu utaifa wa Israel.

Katika vita vilivyofuatia baina ya Waarabu na Israel, kila upande uliazimia kudhibiti maeneo makubwa ya Palestina kadri ilivyowezekana. Kiuhalisia, vita hivyo vilianzisha kufurushwa kwa Wapalestina kutoka maeneo yao, na pale Israel ilipouteka Ukingo wa Magharibi na mji wa Jerusalem mwaka 1967, ndoto ya kuwepo mataifa yale mawili ilionekana kusambaratika.

Mpango huo haukusikika tena hadi mwaka 1980, baada ya jumuiya ya Ulaya kutoa tamko la kutaka Wapalestina wapate haki ya kuamua mambo yao wenyewe, na kutoa rai ya kuundwa kwa mataifa mawili. Ilichukuwa miongo miwili hadi pale Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipoliafiki wazo hilo mwaka 2002.

Marekani yajiunga na wazo la mataifa mawili

George W Bush alikuwa rais wa kwanza wa Marekani kulikubali wazo hilo la mataifa mawili, na wajumbe wa Israel na Palestina walilikubali katika makubaliano ya Geneva mwaka 2003. Msingi wa makubaliano hayo ulikuwa hatua ya chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO kuitambua Israel mwaka 1988. Haikufanya hivyo kwa tamko la moja kwa moja, bali kwa kutangaza nia ya kuunda taifa la Palestina katika ardhi zilizokaliwa na Israel kimabavu mwaka 1967.

Chama cha Hamas pia kiliafiki msimamo huo, japo kupitia kwa kauli binafsi za viongozi wake kama Ismail Haniyeh. Maafisa wengi wa Hamas waliridhia pia, lakini kwa masharti kuwa hatua yoyote ya kuundwa kwa mataifa mawili lazime ipitie katika kura ya maoni inayowashirikisha Wapalestina wote.

Ujenzi wa makaazi ya walowezi waongeza sumu katika uhusiano uliodorora

Ingawa wazo la mataifa mawili lilipata umaarufu miongoni mwa Wapalestina na Waisrael mnamo miaka ya 2000, kitendo cha Israel kuendelea kujenga makaazi ya Walowezi kiliwakasirisha Wapalestina wengi, na kuendelea kupanuka kwa miji ya Wayahudi kunalifanya suluhisho hilo kuonekana kama ndoto ya mchana.

Kutokana na mashambulizi ya Wapalestina, hata miongoni mwa Waisrael uungwaji mkono wa suluhisho la mataifa mawili umeshuka sana. Tatizo ni kwamba hakuna suluhisho mbadala lililopo, kwa sababu Waisrael wengi pia wanapinga suluhisho wa Waisrael na Wapalestina kuishi katika taifa, kwa hoja kwamba hilo litahujumu utambulisho wa Israel kama taifa la Kiyahudi.

 

Mwandishi: Kersten Knipp