1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mapigano Idlib

12 Septemba 2018

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kusitishwa mapigano katika mji wa Idlib, huku operesheni ya majeshi ya serikali ya Syria wakisaidiwa na mashambulizi ya anga ya Urusi ikiendelea.

https://p.dw.com/p/34jvH
USA UN-Sicherheitsrat - Syrienkonflikt - Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Reuters/E. Munoz

Guterres amezitaka pande zote zinazohusika katika vita hivi kuwalinda raia, lakini akiweka msisitizo zaidi kwa wale aliowaita wafadhili watatu wa mchakato wa Astana - mazungumzo yaliyoanzia katika mji mkuu wa Kazakhstan; Urusi na Iran, ambayo wanaomuunga mkono Rais Bashar al Assad na Uturuki inayowaunga mkono waasi.

"Idlib haifai kugeuzwa kuwa eneo la umwagikaji damu. Hatua hiyo itasababisha matatizo makubwa ya kibinaadamu ambayo hayajawahi kutokea katika migogoro nchini Syria. Vita dhidi ya magaidi haviziondolei pande husika majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, takribani watu elfu thelathini wamelazimika kuyakimbia makaazi yao makwao mwezi huu kutoka Idlib kufuatia mapigano hayo. Urusi na Syria awali zilitetea hatua za kuwapeleka wanajeshi wao nchini Syria kwa kusema kwamba wanawalenga magaidi.

Hapo jana, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan De Mistura, alikutana na maafisa wa Urusi, Iran na Uturuki katika juhudi za kupata uungaji mkono wa kuanzisha mazungumzo ya amani kati ya pande zinazotofautiana nchini Syria.  Hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amekataa kuondosha uwezekano wa Ujerumani kuanzisha mashambulizi dhidi ya Syria iwapo serikali ya nchi hiyo itatumia silaha za kemikali kwa waasi eneo la Idlib, lakini akasisitiza kwamba watafanya uamuzi huo kwa uhuru.

Deutschland Berlin Heiko Maas trifft Nikos Christodoulides
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani (mwenye tai nyekundu) Heiko Maas akiwa na Waziri wa Masuala ya Nje wa Jamhuri ya Cyprus, Nikos ChristodoulidesPicha: Iimago/photothek/J. Schmitz

Ikumbukwe Ujerumani haikushiriki mashambulizi ya wanajeshi wa Marekani, Ufaransa na Uingereza nchini Syria mnamo mwezi Aprili mwaka huu, ambayo yalifanyika baada ya tuhuma kuwa wanajeshi wa Syria waliwaua mamia ya watu kwa kemikali za sumu katika mji wa Douma ulio karibu na mji mkuu, Damascus.

Juzi Jumatatu, kitengo cha utafiti cha Bunge la Ujerumani kilisema kwamba hatua ya Ujerumani kukosa kushirikishwa kwenye mashambulizi hayo ilikiuka sheria za kimataifa. Vilevile kilisema kwamba iwapo Ujerumani itajihusiha na mashambulizi ya ulipizaji kisasi katika siku zijazo itakuwa ukiukaji wa katiba ya nchi hiyo, ambayo inasema kwamba nchi hiyo inaweza tu kushiriki katika oparesheni ya pamoja kwa jukumu la kimataifa kama vile kutoka Jumuiya ya NATO, Umoja wa Ulaya au Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo, serikali ya Ujerumani haijazungumzia ripoti hiyo. Hatua ya Ujerumani kusita kujihusisha na masuala ya kijeshi imekuwa ikimkasirisha Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye ameikosoa Ujerumani kwa kushindwa kuafikia malengo ya NATO kuhusu ulinzi na kuilaumu kwa kuiegemea Marekani.

Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE

Mhariri: Mohammed Khelef