1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Mwaka mmoja wa vita umesababisha kiwewe na uharibifu, Gaza

7 Oktoba 2024

Maisha ya Wapalestina wa Gaza yamegeuka tangu mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas huko kusini mwa Israel. Mwaka mmoja baadae, sehemu kubwa za Ukanda wa Gaza zimeharibiwa, na wakaazi hawaoni mwisho wa mapigano hayo.

https://p.dw.com/p/4lUUq
Khan Younis ni moja ya miji mingi ya Gaza ambayo mitaa yake imejaa vifusi
Khan Younis ni moja ya miji mingi ya Gaza ambayo mitaa yake imejaa vifusiPicha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Tangu mashambulizi ya Hamas yalipotokea mwaka uliopita kusini mwa Israel, mambo hayajawa sawa tena kwa wakaazi wa Ukanda wa Gaza. Hadi wakati huo, Israel na Misri zilikuwa zinadhibiti mipaka ya eneo hilo. Lakini majira ya asubuhi ya Oktoba 7, wanamgambo wanaoongozwa na Hamas walirusha roketi kadhaa na kuvunja uzio wa mpaka, wakaingia katikati ya jamii, na kambi za jeshi kusini mwa Israel.

Takribani watu 1,200 waliuawa katika shambulizi hilo, na wanamgambo waliwachukua watu 250 mateka hadi Gaza. Wanajeshi wa Israel walilipiza kisasi siku hiyo hiyo na kufanya mashambulizi makali ya anga katika eneo la Palestina.

Hofu yatanda Gaza

Warda Younis ameiambia DW kuwa mnamo Oktoba 7 waliamshwa kwa milio ya mashambulizi ya roketi. Anasema hali ilikuwa mbaya, na walianza kuangalia taarifa ya habari na kujua kilichotokea, na kuanzia siku hiyo hofu kubwa ilianza na haijaondoka hadi leo.

Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, ambayo haitofautishi kati ya raia na wapiganaji, zaidi ya watu 41,000 waliuawa kwenye eneo hilo mwaka uliopita. Watu wengine 96,000 walijeruhiwa, na takribani 10,000 hawajulikani walipo.

Vikosi vya Israel vikiwa huko Gaza
Vikosi vya Israel vikiwa huko GazaPicha: IDF/Handout/REUTERS

Bidhaa huko Gaza zikaanza kumalizika haraka katika wiki za kwanza za vita, wakati Israel ilipolizingira eneo hilo. Kwa miezi kadhaa, Umoja wa Mataifa umesema mashirika ya kutoa misada yalionya kuhusu uwezekano wa kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza, madai ambayo mamlaka ya Israel imeyakanusha.

''Ilifikia wakati tulikuwa tunakula majani na matawi ya miti, kwa sababu hatukuweza kupata unga au mkate kwa wakati huo,'' alifafanua Younis. Kamwe hawakuwahi kufikiria maisha yao yatageuka na kuwa kama yalivyo sasa.

Wakati misafara ya malori ya misaada ya kwanza ilipowasili kaskazini mwa Gaza, alishuhudia ghasia na vifo kutokana na watu kugombania chakula na msaada.

Katikati ya Oktoba mwaka 2023, jeshi la Israel liliamuru watu wa kaskazini mwa Gaza kuondoka na kuelekea eneo la kusini. Hata hivyo, Younis anasema aliamua kubaki, licha ya kuwa na wanafamilia walioweza kumchukua yeye na watoto wake huko Khan Younis, mji uliopo umbali wa kilomita 8 kutoka mpaka wa Gaza na Misri.

Amjad Shawa (wa tatu kulia), akiwa katika darasa moja huko Deir al-Balah, Gaza
Amjad Shawa (wa tatu kulia), akiwa katika darasa moja huko Deir al-Balah, GazaPicha: privat

Amjad Shawa, aliyekuwa akifanya kazi katika shirika la kiutu linalowakilisha mashirika yasio ya kiserikali ya Kipalestina ameiambia DW kuwa anakadiria takribani watu milioni 1, wanaishi huko Deir al-Balah, huku wengi wakiishi kwenye mahema. Wengine wamefanikiwa kupata nyumba, na wengine wanaishi na ndugu zao.

"Ninaona kwenye nyuso zao. Watu wengi wameumia sana. Wana kiwewe. Wamepoteza kila kitu. Wengi wamepoteza wapendwa wao. Wengi wamepoteza kipato chao, nyumba zao," alielezea Shawa.

Wafanyakazi wa mashirika ya kiutu wako hatarini

Shawa anasema kuwa mfanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada Gaza ni hatari. Anasema wengi wamekufa wakijaribu kuwasaidia wengine. Kwa upande wake, Gaza ambako alizaliwa na kukulia, imeondoka kabisa.

Zaidi ya asilimia 60 ya nyumba za Gaza zilizoharibiwa katika vita vya nyuma, zimeripotiwa kuharibiwa zaidi katika mzozo wa sasa. Shule, hospitali na biashara mbalimbali pia zimeharibiwa.

Baadhi ya wakaazi wa Gaza, akiwemo Rita Abu Sido, wanasema bado hawajui iwapo wataweza kurejea Gaza, kwa sababu kurejea huko inaonekana kuwa changamoto. Abu Sido anasema itachukua muda sana, na kwamba kizazi chao, kizazi kijacho, laziwe kiwe na nia ya kuijenga upya Gaza.

(DW)