1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 yaingilia kati moto wa Amazon

25 Agosti 2019

Viongozi wa mataifa saba yenye uchumi mkubwa wa viwanda, G7, yamekubaliana kwamba nchi zilizoathiriwa na moto unaoendelekea kwenye msitu wa Amazon yanapaswa kupatiwa msaada wa haraka.

https://p.dw.com/p/3OSNv
G7-Gipfel in Frankreich | Donald Trump mit Boris Johnson
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika mjini Biarritz, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, aliwaambia waandishi wa habari kwamba walikuwa wanaendelea kuwasilana na mataifa yote ya Amazonia kupitia timu za mataifa ya hayo G7 ili kujuwa ni ahadi gani za msaada wa kiufundi na kifedha yatowe.

"Urejeshaji wa msitu huo ni muhimu pia lakini kulikuwa na mitazamo tafauti ya viongozi wa G7, kwani yote yanategemeana na mataifa yenyewe na Amazonia, ambayo yana mamlaka ya kisiasa kwenye eneo na hilo linaeleweka," alisema Macron.

Hata hivyo, rais huyo wa Ufaransa alisema kutokana na umuhimu wa msitu huo kwa maisha ya viumbe mbalimbali, hewa ya oksijini na vita dhidi ya kupanda kiwango cha joto ulimwenguni, lazima jitihaza za kuuotesha upya msitu huo zifanyike.

Licha ya kwamba asilimia 60 ya msitu huo imo ndani ya ardhi ya Brazil, mataifa mengine manane ya eneo hilo yanafikiwa na msitu huo mkubwa kabisa wa asili ulimwenguni. Mataifa hayo ni Bolivia, Colombia, Ecuador, Guiana ya Ufaransa, Guyana, Peru, Suriname na Venezuela.

Brasilien Brände im Amazonasgebiet
Moto ukiendelea kuuteketeza msitu mkubwa wa Amazon.Picha: Getty Images/AFP/C. de Souza

Uamuzi wa Macron kuuweka mzozo huo wa Amazon kwenye moja ya ajenda kuu za mkutano wa G7 ulimughadhabisha Rais Jair Bolsonaro wa Brazil, aliyelaani vikali kile alichosema ni uingiliaji kati wa mataifa ya kigeni katika mambo ya ndani ya nchi yake. 

Kiongozi huyo wa siasa kali za mrengo wa kulia alikiita kitendo hicho cha rais wa Ufaransa kuwa ni "akili ya kikoloni."

Mazungumzo na Iran?

Katika hatua nyengine, Rais Macron alikanusha madai kwamba mataifa hayo ya G7 yalikuwa yamempa mamlaka ya kufanya mazungumzo na Iran kwa niaba ya kundi hilo linalotambuliwa kwamba ni nchi zenye demokrasia ya hali ya juu ulimwenguni.

"G7 ni klabu isiyo rasmi, hakuna kitu kama mamlaka rasmi ambayo mtu mmoja humpa mwengine", aliwaambia waandishi wa habari. Badala yake, alisema kiongozi huyo, kwamba angelisaka njia za kuzungumza na Iran kwa niaba ya Ufaransa na kwa kuzingatia majadiliano yake na mataifa ya Magharibi na Japan.

Spanien Gibraltar | In Adrian Darya 1 umbenannter Grace 1 Supertanker
Meli ya mafuta ya Iran baada ya kuachiliwa kutoka mamlaka za Uingereza katika eneo la Gibraltar.Picha: Reuters/J. Nazca

Awali, maafisa wa kidiplomasia wa Ufaransa walikuwa wamenukuliwa wakisema kwamba mataifa ya G7 yalimpa idhini Macron kuzungumza na Iran ili kupunguza hali ya wasiwasi baina yao, lakini Rais Donald Trump wa Marekani akalizima hapo hapo wazo hilo.

Wasiwasi baina ya Iran  na mataifa ya Magharibi umefikria kiwango cha juu katika Ghuba ya Uajemi hivi sasa, wakati Marekani ikiamua kutumia kiwango cha juu ya shinikizo, vikiwemo vikwazo vipya dhidi ya Iran. 

Miongoni mwa hatua za karibuni kabisa za Marekani ni jaribio la kuizuwia meli ya mafuta ya Iran iliyokuwa imeshikiliwa na Uingereza katika eneo la Gibraltar isipite kwenye Bahari ya Mediterenia. 

Meli hiyo iitwayo Adrian Darya 1, ambayo wakati inashikiliwa ilikuwa ikiitwa Grace 1, ilikamatwa kwa siku kadhaa katika eneo la Gibraltar kwa tuhuma kwamba ilikuwa inasafirisha mafuta kuelekea Syria na, hivyo, kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Hadi kufikia Jumapili (25 Agosti) meli hiyo ilikuwa ikielekea mashariki mwa bahari hiyo, huku Ugiriki na Uturuki zikikataa kuiruhusu kutia nanga licha ya awali kukubali ombi hilo la Iran. 

Jeshi la Iran lilisema liko tayari kuisindikiza meli hiyo kurejea nyumbani ikiwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ungelitowa agizo hilo.