1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA yaunda jopokazi kuhusu Dimba la Dunia la Qatar 2022

4 Oktoba 2013

Dimba la kombe la dunia la mwaka wa 2022 nchini Qatar linaendelea kugonga vichwa vya habari kutokana na sababu chungu nzima, na bodi ya maamuzi ya FIFA imekutana ili kulijadili kwa mapana

https://p.dw.com/p/19tqV
Rais wa FIFA Sepp Blatter akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Shirikisho hilo Zurich
Rais wa FIFA Sepp Blatter akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Shirikisho hilo ZurichPicha: Reuters

Pamekuwa na pendekezo la kutaka kuhamisha dimba hilo kutoka miezi ya majira ya joto, ili kuwaepusha mashabiki na wachezaji dhidi ya joto kali…

Na baada ya mkutano wa jana, Rais wa FIFA Sepp Blatter ametangaza kuwa Dimba hilo litaandaliwa nchini Qatar kama tu ilivyopangwa, lakini uamuzi kama kweli litaandaliwa katika majira ya joto utafanywa baada ya dimba la kombe la dunia nchini Brazil. Amesema jopokazi litashauriana na viongozi wa kabumbu na kampuni za matangazo kote ulimwenguni, na kisha kuwasilisha ripoti yake kwa kamati kuu baada ya miezi kadhaa.

Bodi ya Blatter pia inatafuta jibu kuhusu unyanyasaji unaofanywa na Qatar dhidi ya wafanyakazi ambao ni wahamiaji, baada ya kutokea madai ya vifo na ukiukaji wa haki za binadamu katika miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo itakayotumika kwa dimba hilo la dunia.

Picha ya mojawapo ya viwanja vitakavyotumika kwa fainali za kombe la dunia nchini Qatar
Picha ya mojawapo ya viwanja vitakavyotumika kwa fainali za kombe la dunia nchini QatarPicha: picture alliance/Frank Rumpenhorst

Blatter amekuwa akiishawishi FIFA katika miezi ya karibuni, kutaka kubadilisha tarehe za dimba la dunia la 2022…Kamati Kuu ya Qatar 2022 inasisitiza kuwa inaweza kuandaa dimba lililo salama, mwezo Juni na Julai, kwa kutumia tekonolojia ya hewa ya baridi, ijapokuwa itatii amri kama FIFA itaafikiana kwa kauli moja kubadilisha tarehe hizo.

Changamoto za kisheria katika uamuzi wa kuzibadilisha tarehe za dimba hilo zimekuwa zikizungumziwa kwa muda mrefu na nchi zilizoshindwa kupewa haki za kuliandaa, ligi za soka Ulaya zikilazimika kubadilisha ratiba zao za Agosti hadi Mei nazo kampuni za matangazo zikilazimika kununua haki za kurusha matangazo kwa tamasha hilo la Juni hadi Julai.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman