1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

FIFA kuzungumza na wadau wa soka juu ya Kombe la Dunia

20 Septemba 2021

FIFA itafanya mazungumzo na vilabu vya mpira, wasimamizi wa ligi na vyama vya wachezaji kufuatia pendekezo la hivi karibuni la kuandaa michuano ya kombe la dunia kila baada ya miaka miwili.

https://p.dw.com/p/40ZXi
FIFA Fußball-Weltmeisterschaft Katar 2022 | Pokal
Picha: Ulmer/imago images

Shirikisho la soka duniani FIFA litafanya mazungumzo na vilabu vya mpira, wasimamizi wa ligi na vyama vya wachezaji mwezi huu kufuatia pendekezo la hivi karibuni la kuandaa michuano ya kombe la dunia kila baada ya miaka miwili.

Mashirika yote wanachama wa FIFA 211 pia yamealikwa kwenye mazungumzo hayo yatakayofanyika Septemba 30 kwa njia ya mtandao, yakiwa sehemu ya kujadili muundo mpya wa michuano ya kombe la dunia.

FIFA ilipokea maoni mapema mwezi huu kutoka kwa wachezaji wastaafu walioshiriki mkutano wa siku mbili nchini Qatar juu ya pendekezo hilo la kuandaa kombe la dunia kila baada ya miaka miwili.

FIFA pia ilikusanya maoni ya mashabiki wa kandanda kutoka mataifa mbalimbali juu ya suala hilo.

Soma pia: FIFA yakataa kuongeza timu kombe la dunia

Hata hivyo, utaratibu huo wa kukusanya maoni ulikosolewa na muungano wa wachezaji wa sasa FIFPRO ambao pia unatarajiwa kukutana na shirikisho la FIFA kujadili juu ya pendekezo hilo.

"Awamu mpya ya mashauriano" itaanza hivi karibuni inayohusisha wawakilishi wa wachezaji, vilabu na mashirika sita ya soka duniani, FIFA imesema leo Jumatatu katika taarifa.

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limetishia kususia michuano ya kombe la dunia iwapo muundo wake utabadilika kutoka mzunguko wa kila baada ya miaka minne na badala yake kuandaliwa kila baada ya miaka miwili.

UK Arsene Wenger
Meneja wa zamani wa Arsenal Arsene WengerPicha: Matt Crossick/empics/picture alliance

Shirikisho la soka la Amerika ya Kusini CONMEBOL pia limepinga pendekezo hilo.

Mataifa wanachama wa CONMEBOL yanatamba uwanjani lakini idadi jumla ya kura zake ni chini ya theluti moja tu kati ya mataifa 211.

FIFA inaunga mkono pendekezo la kuandaliwa kwa kombe la dunia kila baada ya miaka miwili, ikisema michuano hiyo itatoa fursa kwa wachezaji wengi na timu nyingi kushiriki michuano katika ngazi ya kimataifa na hivyo basi kuongeza ushindani. Pia FIFA imesema michuano hiyo itasaidia kukuza talanta na kukusanya fedha zaidi kwa ajili ya programu za maendeleo ya soka.

Hata hivyo, wapinzani wa pendekezo hilo wanasema litaleta msuguano kati ya soka la kimataifa na ngazi ya klabu, kando na kuwa mzigo mkubwa kwa wachezaji.

Mabadiliko hayo yaliyopendekezwa na FIFA yanaongozwa na Arsene Wenger, meneja wa zamani wa Arsenal ambaye sasa ni mkurugenzi wa kitengo cha maendeleo ya soka FIFA. Wenger amesema uamuzi wa mwisho juu ya pendekezo hilo huenda ukafanywa mnamo mwezi Disemba.