1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yazindua mpango kulinda hospitali dhidi ya udukuzi

15 Januari 2025

Umoja wa Ulaya umetangaza hatua mpya za dharura Jumatano kukabiliana na tishio linaloongezeka kwa hospitali na sekta ya afya kutokana na ongezeko la mashambulizi ya kimtandao.

https://p.dw.com/p/4p9oD

Mashambulizi hayo yanajumuisha uvunjaji wa data au programu za kukomboa fidia (ransomware) – aina ya uhalifu wa kidijitali ambapo wadukuzi hufunga data au kuzuia huduma, wakidai malipo ili kurejesha ufikiaji.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, alionya mwezi Novemba kwamba mashambulizi ya aina hiyo kwenye hospitali yanaweza kuwa "masuala ya maisha na kifo" wakati WHO na nchi takriban 50 zilieleza wasiwasi wao katika Umoja wa Mataifa kuhusu tishio hili linaloongezeka.

Soma pia:Mifumo ya kompyuta Ujerumani yadukuliwa 

Kwa mujibu wa Tume ya Ulaya, kulikuwa na "matukio makubwa ya usalama wa kimtandao" 309 yaliyoathiri sekta ya afya ya EU mwaka 2023 – zaidi ya sekta nyingine yoyote muhimu ndani ya umoja huo.

EU ilionya kuwa hospitali na watoa huduma za afya ni "hatarini zaidi" dhidi ya mashambulizi hayo, ambayo yanaweza kusababisha kuvurugika kwa matibabu na kuhatarisha usalama wa data za wagonjwa.

Hatua zilizopangwa ni pamoja na kuanzisha kituo cha msaada wa usalama wa kimtandao kwa hospitali na watoa huduma za afya kote Ulaya.

FBI yakanusha tuhuma za Trump dhidi ya Obama

Pendekezo hilo linakusudia kuhimiza hospitali kuhakikisha usalama wa data kwa mifumo imara ya kuhifadhi nakala, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi jinsi ya kukabiliana na vitisho vya kimtandao, na kuwasaidia watoa huduma za afya kuepuka kulipa fidia kwa wadukuzi.

Soma pia: India: Makampuni yakabiliwa na mashambulizi ya mtandaoni

EU pia itapanua matumizi ya zana za kufungua programu za kukomboa fidia (ransomware) ili kusaidia kupona kutokana na mashambulizi kama sehemu ya mpango huo unaolenga kulinda huduma zisikatishwe kwa wagonjwa.

Aidha, nchi 27 wanachama wa EU zimetakiwa kuandaa mipango ya kitaifa ya kuimarisha usalama wa kimtandao katika sekta ya afya, kwa kuzingatia hatari maalum katika kila nchi.

Tume hiyo ilisema itajadili zaidi vitisho hivyo na sekta husika ili kuunda mpango "maalum na ulioelekezwa" zaidi ifikapo mwisho wa mwaka.

"Kinga ni bora kuliko tiba, kwa hivyo tunahitaji kuzuia mashambulizi ya kimtandao kabla hayajatokea. Lakini yakitokea, tunapaswa kuwa tayari kuyagundua, kuyakabili na kuyatatua haraka," alisema mkuu wa teknolojia wa EU, Henna Virkkunen, katika taarifa yake.

"Ni lazima wagonjwa wahisi kuwa taarifa zao nyeti ziko salama. Wataalamu wa afya wanapaswa kuwa na imani na mifumo wanayotumia kila siku kuokoa maisha," alisema kamishna wa afya wa EU, Oliver Varhelyi.