Ethiopia kusaidia kupambana na al-Shabaab Somalia
26 Novemba 2011Hapo jana, kwa mara ya kwanza, afisa mmoja wa Ethiopia, alithibitisha kuwa kikosi kidogo kimeshavuka mpaka kwenda Somalia kufanya upelelezi. Afisa huyo ambae hakutaka kutajwa kwa jina amesema, Ethiopia bado haikushiriki kamili katika operesheni za kijeshi. Kwa sasa, vikosi hivyo vinahusika na operesheni za upelelezi. Hata hivyo, vikosi vya Ethiopia vitakuwepo Somalia kwa muda mfupi tu. Hapo awali, Ethiopia ilikanusha kuwa malori kadhaa ya kijeshi yalivuka mpaka kwenda Somalia Novemba 19 na 20. Majeshi ya Kenya yaliyoingia Somalia tangu wiki sita zilizopita kuwashambulia waasi wanaodhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya kusini na ya kati nchini humo, yanakumbana na mvua kubwa na wanamgambo wanaotumia mbinu za wapiganaji wa msituni.
Hapo jana, kwenye mkutano uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, Mkuu wa shirika la maendeleo la nchi za Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, Mahboub Maalim alisema, Ethiopia imeahidi kusaidia harakati za kujaribu kuleta amani na utulivu nchini Somalia. Viongozi wa kanda hiyo wametoa mwito pia kwa Umoja wa Mataifa kubadili mamlaka ya vikosi vya amani vya Umoja wa Afrika (AMISOM) nchini Somalia, ambavyo sasa vinaruhusiwa kufanya operesheni zake ndani ya eneo la mji mkuu Mogadishu tu. Vile vile wanataka kiwango cha idadi ya vikosi hivyo, cha 12,000 kiongezwe hadi kufikia 20,000. Hivi sasa, vikosi hivyo vina wanajeshi 9.800 kutoka Uganda na Burundi.
Mwandishi: Prema Martin/rtre
Mhariri: Mohammed Khelef