1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan barani Afrika

25 Januari 2017

Tanzania, Msumbiji, Madagascar: Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan yuko ziarani barani Afrika. Miongoni mwa masuala makuu ni mzozo kati yake ya mhubiri Gülen na maslahi ya kiuchumi.

https://p.dw.com/p/2WOW5
Afrikareise Erdogan in Tansania
Picha: Getty Images/AFP

Akiwa nchini Msumbiji Recept Tayyip Erdogan alimuomba mwezake Filipe Nyusi siku ya Jumanne ashirikiane naye katika mapambano dhidi ya kiongozi wa kiroho wa Kiislamu Fethullah Gülen. Maneno sawa na hayo aliyatoa kabla wakati alipoizuru Tanzania, akisema katika mkutano wa waandishi habari pamoja na rais John Magufuli, kwamba wanazo taarifa kwamba watu waliojaribu kuipundua serikali yake pia wanaendesha shughuli zao katika mataifa mengine. Mataifa hayo mengine pia ni mataifa ya Afrika, ambako vuguvugu la Gülen linaendesha shughuli zake likiwa na shule zake lenyewe.

Shule za Gülen: Tata lakini zinapendwa Afrika

Katika ziara yake hiyo ya siku tano Erdogan ametaka shule zote zilizo karibu na vuguvugu la Gülen zifungwe. Lakini shule hizo zinapedwa na watu wa tabaka la kati kutokana na kutoa elimu ya kiwango bora kwa gharama nafuu, anasema Ibrahim Bano Barry, mwanasosholojia kutoka chuo kikuu cha Sonfonia nchini Guinea.

Afrikareise Erdogan in Tansania
Rais Erdogan akishikana mkono na rais Magufuli baada ya mkutano wao wa pamoja na waandishi habari katika ikulu ya rais jijini Dar es Salaam, Januari 23, 2017.Picha: Getty Images/AFP

Katika kipidi cha miaka kadhaa iliopita shule nyingi za Uturuki zimeanzishwa karibu kote barani Afrika, na nyingi ya shule hizo zina mafungamano na vuguvugu la Gülen. Ufuk Tepebas kutoka kituo cha utafiti wa Afrika katika chuo kikuu cha Basel anaonya juu ya uwezekano wa kuzuka mzozo kati ya Uturuki na mataifa ya Afrika kutokana na matakwa ya Erdogan.

"Serikali ya Uturuki inapaswa kuliendea suala hili kwa uangalifu mkubwa na kufuata mkakati wa uvumilivu, kutoa ushahidi wa kutosha na suluhisho mbadala ili kuwashawishi marafiki zake wa Kiafrika. Vinginevyo baadhi ya mataifa ya Kiafrika yanaweza kulichukulia jambo hilo kama kushurutishwa na hilo linaweza kusababisha mzozo katika uhusiano baina yake na mataifa hayo," alisema Tepebas katika mahojiano na DW.

Masoko mapya kwa bidhaa za Uturuki

Hata hivyo uhusiano na Tanzania unaonekana kutoingia madoa mpaka wakati huu. Rais Magufuli amemuomba Erdogan kuipatia nchi hiyo mkopo wa uwekezaji katika ujenzi wa reli kuanzia jiji la Dar es Salaam hadi nchini Zambia. Reli hiyo itaiunganisha Tanzania na mataifa ya Burundi, Uganda and Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, na upo uwezekano mkubwa wa kampuni ya Kituruki kushinda zabuni ya ujenzi wa reli hiyo. Mataifa mengine wahisani yalijitoa katika ufadhili wa mradi huo kufuatia kashfa ya rushwa ya mwaka 2015.

Afrikareise Erdogan in Mosambik
Rais Erdogan na mke wake Emine Erdogan wakiwasalimia wananchi wakati wa sherehe mjini Maputo, Msumbiji, Januari 24, 2017.Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Ozer

Lakini Kristian Brakel kutoka wakfu wa Kijerumani wa Heinrich Boell mjini Istanbul anaona maslahi ya kiuchumi kuwa kiini cha ziara ya Erdogan barani Afrika. Anasema Uturuki inataka kwanza ya yote kutafuta masoko mapya kwa ajili ya makampuni yake ya kiwango cha chini na kati, masoko ambayo yamevurugika kwa sehemu kubwa katika eneo la mashariki ya kati, kwa mfano nchini Syria na Iraq ambako kuna migogoro ya kivita.

"Ni kweli kwamba vuguguvu la Gülen linapaswa kuzuwiwa kwa namna yoyote ile. Serikali ya Uturuki inawatia kishindo kikubwa washirika wa Kiafrika. Lakini kiukweli hilo siyo lengo la msingi, hata kama vyombo vya habari vinaonyesha hivyo," alisema Brakel.

Chini ya utawala wa chama cha Erdogan cha AKP, Uturuki imejenga uchumi imara wa kiwango cha kati. Tabaka hili la wafanyabiashara linakiunga mkono chama cha AKP, anasema Brakel, na kwa sababu hii ndiyo maana Erdogan anataka kuweka mizizi barani Afrika.

Mwandishi: Harjes Christine

Tafisiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Josephat Charo