1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

England yaitandika Sweden bao 4-0 mchezo wa nusu fainali

Sylvia Mwehozi
27 Julai 2022

England watakuwa wakijaribu kushinda kombe la kwanza la michuano mikubwa ya wanawake katika fainali itakayofanyika uwanja wa Wembley mwishoni mwa juma hili.

https://p.dw.com/p/4EgvH
UEFA Women's Euro 2022 I England v Schweden
Picha: Danny Lawson/IMAGO

Mabao ya England yaliwekwa kimiani na wachezaji Beth Mead, Lucy Bronze, Alessia Russo na Fran Kirby. Mchezaji Beth Mead alitangulia kuchungulia nyavu za Sweden kwa kufunga bao la kwanza likiwa ni goli lake la sita katika mashindano hayo ya wanawake. Mead anakuwa mchezaji wa pili kufunga magoli sita katika michuano ya Euro ya wanawake baada ya Inka Grings wa Ujerumani mwaka 2009.Euro 2022 kwa wanawake yatinga nusu fainali

Lucy Bronze alifunga bao la pili la kichwa katika dakika ya 48 ya kipindi cha pili kutoka kona ya kushoto. Mchezaji wa akiba, Alessia Russo alipachika bao la tatu na bora kwa usiku wa jana baada ya mpira uliokuwa umeokolewa awali na mlinda mlango wa Sweden, Hedvig Lindahl. Fran Kirby alihitimisha kapu la magoli ya England na kuihakikishia nafasi ya kutinga fainali.

UEFA Women's Euro 2022 I England v Schweden
Mshambuliaji wa kati wa England Fran Kirby(kulia) akipachika bao la nne Picha: Lindsey Parnaby/AFP

England imetinga fainali ya michuano ya euro kwa upande wa wanawake kwa mara ya tatu, baada ya mwaka 1984 na 2009.  Hata hivyo imepoteza mara zote mbili na haijawahi kushinda mechi kubwa ya mashindano ya kimataifa.

Timu ya wanawake ya Sweden ambayo inashikilia nafasi ya pili duniani kwa ubora nyuma ya  Marekani, ilitarajiwa kutoa ushindani mkubwa kwa England katika mechi hiyo, lakini ilionekana kukosa mbinu za ushambuliaji dhidi ya kikosi cha England kinachonolewa na kocha Mholanzi Sarina Wiegman. Sweden, ilipata nafasi tatu kubwa za kuongoza mapema lakini hazikuzaa mabao.

Nusu fainali ya pili itafanyika baadae usiku wa leo kati ya Ujerumani na Ufaransa na mshindi atapambana na wenyeji England katika fainali itakayofanyika Jumapili katika uwanja wa Wembley.

Kama ilivyofanya timu ya wanaume ya England katika michuano iliyopita ya euro 2020 wakati ilipofikia fainali ya michuano hiyo katika uwanja wa Wembley lakini ilitolewa kwa mikwaju na Italia.

Takribani mashabiki 87,000 wanatarajiwa kuujaza uwanja wa Wembley ikiwa ni rekodi kubwa na kuna matumaini makubwa kwamba England ambayo ni wenyeji, itahitimisha kiu ya muda mrefu ya ubingwa wa mashindano makubwa kwa upande wa wanawake na wanaume. Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limesema kuwa idadi ya watazamaji wa michuano hiyo ya wanawake imeongezeka kulinganisha na mashindano yaliyopita