1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dwamena wa Ghana afariki dunia baada ya kuzimia uwanjani

13 Novemba 2023

Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ghana Raphael Dwamena amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 28 baada ya kuanguka uwanjani nchini Albania.

https://p.dw.com/p/4YjcZ
Raphael Dwamena | ghanaischer Fußballspieler
Picha: Daniel Marzo/Pacific Press/picture alliance

Dakika ya 23 ya mchezo wa ligi ya Albania Superliga kati ya FK Egnatia na Partizani, Dwamena alianguka uwanjani na kufariki dunia siku ya Jumamosi.

Mchezaji huyo wa zamani wa shule ya kandanda ya Red Bull Salzburg, ambaye alicheza mechi tisa za Ghana kati ya 2017 na 2018, alitolewa nje ya uwanja na licha ya majaribio ya kumfufua, baadaye alitangazwa kufariki.

Maisha ya mshambuliaji huyo mwenye kipaji yalitatizwa na matatizo ya moyo na, licha ya wito wa kumtaka astaafu mapema, Dwamena hakuweza kujiondoa kwenye mchezo alioupenda.

Soma pia: Wolfsburg yaomboleza kifo cha Malanda

Dwamena alianza kucheza soka katika klabu ya Red Bull Ghana kabla ya kuhamia Austria kuchezea Salzburg. Lakini ilikuwa huko Austria Lustenau na kisha FC Zürich ambapo Dwamena alijitangaza kuwa mshambuliaji bora, akifunga mabao 21 katika mechi 51 katika msimu mmoja wa 2017-18.

Historia ya ugonjwa wa moyo

Spanien Fußball 2019 | Raphael Dwamena, von Levante UD
Raphael DwamenaPicha: David Aliaga/MB Media/IMAGO

Maisha ya Dwamena yaliathirika na ugonjwa wa moyo ambao uligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2017. Mwaka huo, alitarajia kuhamia katika klabu ya Ligi ya Premia ya Brighton nchini England ambayo angesajiliwa kwa thamani ya € 11.4 milioni, lakini ilishindikana alipofeli vipimo vya matibabu kutokana na matatizo ya moyo wake.

Mnamo 2020, akiwa katika klabu ya Levante ya Uhispania, aliwekewa kifaa cha kupandikizwa cha moyo na mishipa (ICD), kama alichowekewa Christian Eriksen baada ya mshtuko wa moyo uwanjani mnamo 2021, ambacho pia huwekwa kwa wachezaji wengine wenye magonjwa ya moyo.

Kifaa hicho kiliwawezesha madaktari wa klabu ya Levante kufuatilia moyo wake wakati wa michezo. Mnamo Oktoba 2020, kufuatia kuhamia katika ilabu ya Denmark Vejle Boldklub, alizuiwa kuingia uwanjani baada ya kifaa alichopandikiziwa kuonyesha matokeo ambayo yalionekana kuwa ya juu sana.

Mwaka mmoja baadaye mnamo Oktoba 2021, Dwamena alirejea Austria akiichezea Blau-Weiss Linz, na wakati wa mechi alizimia tena na kifaa chake cha ICD kikamsaidia kuzinduka tena lakini mchezo uliahirishwa na kibarua chake huko Austria kumalizika.

Miito ya kustaafu

Raphael Dwamena | ghanaischer Fußballspieler
Picha: Daniel Marzo/Pacific Press/picture alliance

Kulikuwa na wito wa mara kwa mara wa kumtaka Dwamena kustaafu soka, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa daktari kutoka Ghana, Prince Pambo, ambaye mnamo Novemba 2021, muda mfupi baada ya Dwamena kuzimia huko Austria, alimtaka mshambuliaji huyo kufikiria kujipa muda kando na maisha yake ya uchezaji.

Dwamena hakusikiliza wito huo mnamo 2023, alitafuta klabu ya Albania inayoshiriki katika Superliga FK Egnatia na kuanza tena kucheza soka. Mambo yalikuwa yamemwendea vyema mshambuliaji huyo mwenye kipaji, ambaye alifunga mara 20 katika mechi 28, na kuifanya klabu yake kuwa kileleni mwa jedwali.

Lakini Jumamosi, Novemba 11, katikati ya kipindi cha kwanza cha mchezo kati ya vilabu viwili vikuu vya Albania, Dwamena alianguka na kufariki dunia, huku kifaa chake cha ICD kikishindwa kumuokoa wakati huu.
 

//https://p.dw.com/p/4YhmC