1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfrika Kusini

Duru zasema ANC imemfukuza Zuma chamani

29 Julai 2024

Kamati ya nidhamu ya chama tawala nchini Afrika Kusini cha ANC imeamua kumvua uanachama na kumfukuza chamani rais wa zamani Jacob Zuma kwa kuongoza chama hasimu katika uchaguzi uliofanyika mwezi Mei.

https://p.dw.com/p/4iqHz
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma
Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma. Picha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Hayo yameripotiwa na vyombo kadhaa vya habari nchini Afrika Kusini vikinukuu nyaraka iliyovuja kutoka kwenye vikao vya kamati ya chama hicho. Nyaraka hiyo ambayo pia shirika la habari la AFP limeiona inasema Zuma amefukuzwa lakini anayo haki ya kukata rufaa katika kipindi cha siku 21.

Mnamo mwezi Januari, mkutano mkuu wa ANC ulimsimamisha uanachama Jacob Zuma ikiwa ni mwezi mmoja baada ya mwanasiasa huyo kutangaza kukiunga mkono chama kipya kilichokuwa kimeundwa cha  uMkhonto weSizwe (MK).

Chama hicho kilifanya vizuri katika uchaguzi wa Mei 29 kwa kunyakua asilimia 14.5, matokeo yaliyokinyima ushindi mkubwa wa ANC na kukilazimisha kwa mara ya kwanza kuunda serikali ya mseto.