1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund yapanda hadi nafasi ya pili

19 Februari 2018

Marco Reus alifunga bao lake la kwanza la Bundesliga tangu mwezi Mei na kuipa Borussia Dortmund ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Borussia Moenchengladbach

https://p.dw.com/p/2svj9
Fußball Bundesliga Borussia Mönchengladbach vs Borussia Dortmund | Jubel
Picha: Getty Images/Bongarts/C. Koepsel

 Ushindi huo umewaweka BVB katika nafasi ya pili ya msimamo wa Bundesliga na pointi 40 huku Gladbach ikibaki katika nafasi ya 10. Kocha wa Gladbach Dieter Hecking aliwapongeza vijana wake licha ya kichapo hicho

Nadhani tumeshuhudia mchezo mzuri kutoka timu zote mbili kwenye uwanja ambao haukuwa rahisi kucheza. Niliona fursa nzuri leo na pia kwa sababu kwa maoni yangu tulicheza mchezo mzuri. Nnawahurumia sana vijana wangu kwa sababu ya ukosoaji. Ndio sasa nnapojaribu kuwatetea na kuwajenga ili kuwa tayari kuendelea kupambana tena kwa sababu timu ina uwezo mzuri.  

Katika mechi nyingine ya jana, bao la Mario Gomez lilitosha kuipa Stuttgart ushindi dhidi ya Augsburg ukiwa ni wao wa kwanza ugenini msimu huu. Ushindi huo umeiweka Stuttgart juu ya eneo la timu tatu za mkiani na pengo la pointi tatu.

Siku ya Jumamosi, Robert Lewandoswki alifunga penalti katika dakika ya 91 na kuiokoa Bayern Munich na ushindi wa 2-1 dhidi ya Wolfsburg na kuimarisha udhibiti wao kileleni na pengo la pointi 19. Robin Knoche ni mchezaji wa Wolfsburg na hapa anaelezea kusikitishwa kwake na kichapo hicho

Fußball: 1. Bundesliga, 23. Spieltag | Hamburger SV - Bayer Leverkusen
Leon Bailey aliendelea kutambaPicha: picture-alliance/dpa/C. Charisius

Nadhani ukiangalia juhudi tulizofanya, tulikuwa na mchezo mzuri sana kwa dakika 90 na kisha tukaadhibiwa kwa kosa moja tu tulilofanya dhidi ya Bayern. Na inauma sana kwamba hatukupata chochote. Tulipanga mchezo wetu kuwa wa kujilinda kwa bidii, tukafungabao na kuonyesha tuna uwezo. Ndio tuliwaachia mchezo Bayern, hilo linaweza kutokea wakati mwingine kwa timu nyingine 16 za Bundesliga. Kama tu nilivyosema, mwishowe, utaadhibiwa na kosa moja tu.

RB Leipzig wanacheza leo dhidi ya Eintracht Frankfurt katika mchuano wa kwanza kuwahi kuchezwa Jumatatu usiku katika Bundesliga. Hivyo Bayer Leverkusen waliitumia nafasi hiyo kwa kusonga hado nafasi ya tatu kwa kuilaza Hamburg 2-1. Kevin Volland ni mshambuliaji wa Leverkusen

Tumecheza vizuri sana. Tuliyazuia kabisa makombora na mwishowe tukashinda. Labda kulikuwa na hali moja au nyingine ambayo ilikuwa ngumu kwetu. Lakini pia tulikuwa na mashambulizi kadhaa. Ulikuwa ni ushindi mgumu na tuna furaha kuwa tulishinda kabla ya mchuano wa wiki ijayo dhidi ya Schalke. Ushindi huu ulikuwa muhimu sana kwetu 

Schalke ilipanda hadi nafasi ya tano baada ya ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Hoffenheim. Katika matokeo mengine, Freiburg ilipata ushindi wa moja bila dhidi ya Werder Bremen. Washika mkia Cologne walitoka sare ya 1-1 na Hanover

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu