1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dortmund wafalme wa dabi ya Ruhr

18 Mei 2020

Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga hatimaye ilirejelea mechi zake mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya maambukizi ya virusi vya corona kupungua Ujerumani. Jumla ya mechi nane zilipigwa ila hakukuwepo mashabiki viwanjani.

https://p.dw.com/p/3cQX0
Deutschland Bundesliga BVB gegen Schalke | Tor Haaland
Picha: Reuters/M. Meissner

Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga hatimaye ilirejelea mechi zake mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya maambukizi ya virusi vya corona kupungua nchini humu. Jumla ya mechi nane zilipigwa katika viwanja tofauti ila hakukuwepo mashabiki katika viwanja vyote. Kubwa kati ya mechi hizo ilikuwa ile mama wa dabi zote, Borussia Dortmund dhidi ya Schalke 04 katika uwanja wa Signal Iduna Park.

Safari hii Dortmund walilipiza kisasi kwa kuwalemea hao mahasimu wao 4-0 baada ya msimu uliopita kufungwa 4-2 hapo hapo nyumbani kwao. Mshambuliaji chipukizi wa Dortmund Erling Haaland ndiye aliyepachika wavuni goli la kwanza kisha Raphael Guerreiro akafunga mawili na Thorgan Hazard akapata bao moja na kuyapelekea magoli hayo kuwa mane.

Deutschland Bundesliga BVB gegen Schalke | Jubel Guerreiro
Julian Brandt akisherehekea na Raphael Guerrero aliyefungaPicha: Reuters/M. Meissner

Baadhi ya mabadiliko ambayo yameshuhudiwa baada ya mechi kurudi Ujerumani, ni timu kukubaliwa kubadilisha wachezaji watano badala ya watatu kama ilivyo ada. Baadhi ya makocha wamefurahishwa na hatua hiyo, huyu hapa Lucien Favre kocha wa Borussia Dortmund.

"Ni wazo zuri kubadilisha wachezaji watano, ni muhimu sana kwasababu si timu zote ziko katika kiwango cha juu cha mchezo, timu zitarudi kwenye kiwango hicho polepole. Hatujacheza mechi zozote za kirafiki bila shaka na nafikiri hili ni jambo zuri. Ni muhimu," alisema Favre.

Ingawa mashabiki hawakuwepo uwanjani, wengi walizitazama mechi hizo kwenye mikahawa, kama huyu shabiki wa Dortmund.

"Dabi ni mechi yenye kuleta furaha sana na ukiwa uko na marafiki hata wakiwa ni wachache bado ile furaha ipo. Sasa hivi kwa vile timu yetu inaongoza kwa magoli matatu nafikiri mambo ni mazuri, bila shaka si sawa na kuwa uwanjani palipo na mashabiki 83,000 lakini matokeo yametuliwaza kidogo," alisema Raphael Lewandowski.