Djokovic ndiye mchezaji tenisi mwenye mataji mengi zaidi
12 Juni 2023Novak Djokovic sasa anasimama peke yake miongoni mwa wachezaji walionyakua mataji 23 ya Grand Slam. Baada ya miaka yote hiyo akiwafukuzia wapinzani wake Roger Federer na Rafael Nadal, Djokovic sasa yuko kileleni mwa orodha ya mtu aliyewahi kushinda mashindano mengi Zaidi makubwa. Mserbia huyo alifanya hivyo kwa kumbwaga Casper Ruud hapo jana kwa seti za 7-6, 6-3 7-5 katika fainali ya French Open.
Djokovic sasa amewapiku Nadal ambaye ana mataji 22 na Federer na 20. Hata hiyo Djokovic mwenye umri wa miaka 36 amesema haoni kama ni sawa aitwe mchezaji bora wa muda wote. "Sitaki kusema kuwa mimi ndiye bora zaidi, kwa sababu nahisi nimesema hapo kabla, kuwa ni kuwakosea heshima mabingwa wote katika enzi tofauti za mchezo wetu ambao ulichezwa katika mbinu tofauti kuliko unavyochezwa leo. Kwa hiyo nadhani kila bingwa wa enzi yake aliacha alama kubwa, sifa, na kupisha njia kwa sisi kuweza kucheza mchezo huu katika jukwaa bora kote ulimweguni."
Taji la French Open lilikuwa lake la 3, kando na mataji 10 ya Australian Open, 7 ya Wimbledon na matatu ya US Open. Na alipoulizwa kama anaweza kushinda taji la 24 au 25, alijibu, mbona asiweze? 11 kati ya mataji yake ya Grand Slam yamepatikana tangu alipofikisha umri wa miaka 30.
Mwisho wa michezo kwa sasa, unaweza kusoma mengi Zaidi kwenye tovuti yetu ya dw.com/Kiswahili. Mimi ni Bruce Amani kwaheri.
afp