1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Deschamps: Imani ilitupelekea kuibwaga Uhispania

11 Oktoba 2021

Kocha wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps, amesema imani ndiyo iliyoifanya timu yake iibuke na ushindi wa taji la nations League Jumapili baada ya kutoka chini bao moja na kuilaza Uhispania 2-1 katika fainali.

https://p.dw.com/p/41XZ8
Nations League Finale Frankreich Spanien
Picha: Luca Bruno/AP Photo/picture alliance

Deschamps anasema wamepambana na timu ya Uhispania ambayo ingawa iliwakosa baadhi ya wachezaji wake muhimu, bado ni timu nzuri inayoweza kuisumbua timu yoyote ile duniani.

"Hatukupoteza imani licha ya kupata matokeo yasiyoridhisha kwenye mechi zilizopita, kama hatungekuwa na imani kwenye mechi hizo, singekuwa hapa Milan kucheza fainali na bila shaka hatungeshinda Nations League kama tungekuwa hatujiamini," alisema Deschamps.

Fußball WM 2018 Dänemark v Frankreich
Kocha wa Ufaransa Didier DeschampsPicha: Getty Images/AFP/F. Fife

Kwa upande wake kocha wa Uhispania Luis Enrique anasema anajivunia sana vijana wake licha ya kupoteza fainali ya jana. Kocha huyo ameongeza kwamba wanakimaliza kinyang'anyiro hicho bila majuto ya aina yoyote yale.

Enrique anadai kutokana na jinsi walivyocheza katika fainali ya jana, sasa atakuwa na wakati mgumu sana kuchagua kikosi cha kwanza katika mechi zao zijazo.

"Kama kawaida, haijalishi tunayecheza naye, Uhispania itacheza mchezo wao tu. Tunaweza kucheza vizuri au vibaya bila shaka ila nafikiri mashabiki wote watakubali kwamba Uhispania hucheza vile vile tu. Na ndio maana ni fahari kubwa na ninaridhika na kile nilichokiona katika mashindano haya," alisema Enrique.