DAR ES SALAAM: Rais Mbeki ateuliwa kuwa mpatanishi wa mgogoro wa Zimbabwe
30 Machi 2007Viongozi wa kamati ya maendeleo ya mataifa ya eneo la kusini mwa Afrika, SADC, wametoa mwito vikwazo dhidi ya Zimbabwe viondolewe, licha ya utawala war ais Robert Mugabe kuendelea kukosolewa vikali.
Tangazo hilo lilitolewa na viongozi wa nchi 14 wanachama wa SADC, baada ya kumalizika mkutano wa dharura wa siku mbili uliofanyika mjini Dar es Salaam Tanzania. Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete, alisema viongozi wa SADC wamemchagua rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini aongoze juhudi za kuleta maridhiano baina ya vyama vinavyohasimiana nchini Zimbabwe.
´Uamuzi uliofikiwa ni kuendeleza mdahalo wa vyama nchini Zimbabwe. Hakuna chaguo lengine kwa sababu ni njia ya mdahalo itakayoweza kusuluhisha tofauti baina ya vyama ndani ya Zimbabwe. Kwa hiyo uamuzi uliopitishwa ni kumkabidhi rais Thabo Mbeki kibarua cha kuongoza mchakato wa kuendeleza mdahalo nchini Zimbabwe.´
Mataifa ya magahribi yakiongozwa na Uingereza na Marekani yalikuwa na matumaini ya mkutano huo kulaani hatua ya rais Mugabe ya kukikandamizi chama cha kikuu cha upinzani, Movement for Democtratic Change, MDC, na kukamatwa kwa kiongozi wa chama hicho Morgan Tsvangirai.
Chama cha MDC kimetangaza leo kwamba kiko tayari kukutana na chama tawala cha rais Robert Mugabe, ZANU-PF, lakini kikasema hakitarajii mazungumzo hayo kumaliza mzozo wa kisiasa na kiuchumi nchini Zimbabwe. Ujerumani inayoshikilia urais wa Umoja wa Ulaya imetaka umoja huo uiwekee vikwazo vikali zaidi Zimbabwe.
Rais Mugabe leo hii anatarajiwa kukiongoza chama chake kuidhinisha uchaguzi wa mwaka ujao ambao huenda ukashuhudia kiongozi huyo akigombea wadhifa wa urais kwa awamu nyengine.